Polisi yaituliza Namungo kwao

Namungo imekubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Majaliwa Ruangwa mkoani Lindi.

Huo unakuwa ushindi wa kwanza kwa Polisi Tanzania msimu huu baada ya mechi ya kwanza iliyofanyika Septemba 7 kuchapwa na Azam bao 1-0.

Bao la maafande hao lilifungwa dakika ya 76 na Rashid Juma aliyefunga kwa shuti kali la umbali wa mita 20 lililomshinda kipa wa Namungo Nurdin Balora.

Maafande hao sasa wamefikisha pointi tatu na kupanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.

Polisi Tanzania itashuka tena dimbani Septemba 18 kucheza na maafande wenzao wa JKT Tanzania katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi kuanzia saa 8:00 mchana.

Nayo Namungo itakuwa ugenini kucheza na Prisons katika mchezo utakaofanyika Septemba 19 saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa Nelson Mandela Rukwa.