Polisi Tanzania yaanza na Biashara

Monday July 13 2020

 

By Yohana Challe

LIGI Kuu Tanzania Bara, inaendelea kesho Jumanne kwa michezo mitatu kuchezwa huku Polisi Tanzania ikiwa ugenini dhidi ya Biashara United, Uwanja wa Karume, Mara.

 Ofisa Habari wa timu hiyo, Frank Likwaro amesema wachezaji wametoa ahadi ya kuhakikisha wanapata ushindi ili kukaa nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.

"Wachezaji wanatambua umuhimu wa mchezo dhidi ya Biashara, hivyo kila mmoja atajituma kuhakikisha kuwa timu inapata ushindi ili iweze kujiweka katika mazingira salama na kufikia malengo yao ya kumaliza nafasi ya tano,".

 Hata hivyo, Pato Ngonyani ambaye ni mchezaji wa timu hiyo anasema "Hatutawaangusha mashabiki zetu katika michezo inayofuata na tunaanza na Biashara, mchezo utakuwa mgumu lakini tumeshikamana na kusahau matokeo ya nyuma,".

 Ameongeza kuwa ushindi utaifanya timu hiyo kujiweka katika nafasi ambayo wamelenga kukaa baada ya mwisho wa msimu.

Polisi Tanzania inashika nafasi ya sita ikiwa na alama 48 wakati Biashara ikiwa nafasi ya tisa baada ya michezo 34 ikivuna alama 46.

Advertisement

Michezo mingine ya kesho Ruvu Shooting atacheza na Mwadui FC, Lipuli FC akicheza na KMC.

Advertisement