Polisi Tanzania, yaitangazia Arusha United vita ya FDL

Muktasari:

  • Timu ya Arusha united inajitupa uwanjani wakiwa wamepoteza mechi moja na kutoka suluhu mechi moja kwenye Ligi Daraja la Kwanza huku Polisi Tanzania wakitoka suluhu mechi mbili, na kufungwa moja na leo Alhamisi timu hizo zinakutana katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.


TIMU ya Polisi Tanzania leo Alhamisi itakuwa ugenini kukipiga na Arusha United katika dimba la Sheikh Amri Abeid ukiwa mchezo wa sita kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL) huku Kocha Mkuu, Issah Rugaza akisema anataka pointi tatu kutoka kwenye uwanja huo.

Mpambano huo uliokuwa upigwe Jumapili ya Novemba 11 umerudishwa nyuma kutokana na uwanja huo unaomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa na shughuli nyingine za kijamii kuanzia kesho Ijumaa.

Rugaza alisema amepokea mabadiliko hayo kwa mikono miwili na hawezi kubadilisha azma yake ya kuvuna alama tatu ugenini.

“Unajua timu nyingi hazina viwanja, hivyo wamiliki ndio wanajukumu la kuona umuhimu wa ligi hii na kutupatia nafasi ya kucheza, hivyo kama wameamua kuturuhusu tucheze kesho (leo) sisi hatuna neno ili mradi tu kikosi kiko imara,” alisema Rugaza.

Aliongeza baada ya kupata sare na wapinzani wao Pamba FC wanaoongoza kundi B’ kwa pointi 10, ni wakati wao wa kuvuna alama tatu dhidi ya wenyeji wao Arusha United ili kukaa kileleni mwa kundi hilo kama watafanikiwa kuvuna alama tatu kwenye mchezo wa leo.