Polisi Tanzania: Waliomteka Mo Dewji walitaka fedha

Muktasari:

Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro amesema waliomteka mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ walitaka kupewa fedha licha ya kutotaja kiwango wanachohitaji

Dar es Salaam. Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Tanzania, Simon Sirro amesema waliomteka mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ walitaka kupewa fedha licha ya kutotaja kiwango wanachohitaji.

Sirro ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Oktoba 20, 2018 katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam ambako watekaji hao walimtupa bilionea huyo, kuendelea kuwasisitiza wananchi kutoa taarifa ili watekaji hao wakamatwe.

“Hii gari imetelekezwa na Mo Dewji ameachiwa lakini mwenyewe amesema wazi kuwa waliomteka waliomba fedha ila hawakusema ni kiasi gani,” amesema Sirro.

 “Ila Mo Dewji amesema waliomteka walikuwa na wasiwasi na amesema kuwa walizungumza na baba yake (Gullam Dewji-baba mzazi wa Mo Dewji). Pia ameeleza jinsi walivyomchukua pale hotelini (Colosseum) na kumpeleka sehemu ambako walimfungia.”

Amesema kwa jinsi polisi walivyokuwa wamejipanga watekaji hao wasingeweza kurudi walikotoka na wakaona njia pekee ni kulitelekeza gari lao na kumuachia Mo Dewji.

“Walitelekeza gari saa saba usiku (leo) na Mo aliwasiliana na baba yake ambaye alikuja kumchukua na tulivyokagua gari tulikuta lina silaha nne, bastola tatu, bunduki ya kivita aina ya AK 47 na risasi 19,” amesema Sirro.

Amesisitiza, “Hii ni AK 47 ni salaha ya kivita na kuna uwezekano wametoka nayo kwao ili kuja kuwapa shida Watanzania. Mo ametekwa kwa silaha nne na kama (watekaji) walizoea katika nchi zao sio Tanzania.”

Amesema watekaji hao pia walijaribu kulichoma moto gari hilo, lakini walishindwa na kuamua kulitelekeza.

Sirro alitumia nafasi hiyo kuwaonya watu mbalimbali waliotoa maoni yao kupitia mitandao ya kijamii wakipingana na maelezo aliyoyatoa jana juu ya ulipofikia uchunguzi wa tukio la kutekwa kwa bilionea huyo.