Polisi TZ yaipunguza kasi KMC

MCHEZO wa raundi ya tano Ligi Kuu bara kati ya KMC na Polisi Tanzania umemalizika kwa Polisi kuibuka na ushindi wa bao 1-0, ugenini kwenye uwanja wa Uhuru, Dar.

 

Licha ya KMC kulishambulia mara kwa mara lango la Polisi Tanzania katika kipindi cha kwanza lakini timu zote mbili zilienda mapumziko ubao wa matokeo ukisomeka 0-0.

 

Katika kipindi cha kwanza KMC walikuwa wameutawala mpira kwa kutengeneza nafasi lakini umakini katika umaliziaji ndio ulikuwa changamoto.

 

Dakika ya 9 Reliants Lusajo alitaka kuiandikia bao la kuongoza KMC, alipiga shuti kali akipokea pasi ya Paul Peter lakini kipa wa Polisi Tanzania, Geofrey Mkumbo aliudaka kwa umakini mpira huo.

 

KMC walikuwa wakionyesha kuhitaji goli la mapema kwa kuliandama lango la Polisi na dakika ya 12 Kenny Ally alitaka kuifungia bao KMC lakini umakini ulikosekana baada ya kupiga shuti na kutoka nje kidogo ya goli.

 

Umakini wa washambuliji wa KMC ulikuwa hafifu licha ya kutengeneza nafasi nyingi ndani ya dakika 20 za kipindi cha kwanza.

 

Kwa upande wa Polisi Tanzania, washambuliaji wake Tariq Seif na Marcel Kaheza walikuwa na kazi ngumu katika kupenya safu ya ulinzi ya KMC iliyokuwa ikiongozwa na Andrew Vicent 'Dante' ambaye alikuwa akionekana akifata maelekezo ya kipa wake Juma Kaseja kwa umakini wa hali ya juu.

 

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana kwa awamu huku mbinu za makocha na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja kuonekana zaidi.

 

Baada ya dakika 10, za kipindi cha kwanza Makocha wa timu hizo mbili, Malale Hamsini (Polisi Tanzania) na John Semkoko (KMC) walifanya mabadiliko kwa kumtoa Tariq Seif na nafasi yake kuchukuliwa na Pius Buswita kwa upande wa Polisi Tanzania huku KMC akitoka Paul Peter na kuingia Hassan Kabunda.

 

KMC waliendelea kufanya mabadiliko kwa kumtoa George Mpole dakika ya 69 na nafasi yake kuchukuliwa na Ramadhan Kapera na dakika ya 75 alitoka Yusuph Mvuyekure na kuingia Mohammed Samata.

 

Dakika ya 82 mabadiliko mengine kwa timu zote mbili kwa kumtoa Rashid Juma na nafasi yake kuchukuliwa na Hamad Said huku na kwa KMC akaingia Martin Kigi aliyechukua nafasi ya Abdul Hillary.

 

Dakika ya 88, Polisi Tanzania walipata bao la kuongoza na la ushindi kupitia kwa Pius Buswita aliyeingia kipindi cha pili baada ya kutokea sintofahamu kwa mabeki wa KMC.

 

Ushindi huo unawafanya Polisi Tanzania kufikisha pointi 10, na kupanda mpaka nafasi ya 4 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara.

 

KMC inakuwa mechi ya pili mfululizo kupoteza baada ya kufungwa bao 1-0 na Kagera Sugar ugenini hivyo wanasalia na alama 9 wakishinda mitatu na kupoteza miwili huku Polisi Tanzania ikipaa hadi nafasi ya 4 kutoka ya 6.