Pole kwa Thierry Henry na Roy Keane

Saturday November 24 2018

 

By EDO KUMWEMBE

ILIANZIA kwa Gary Neville, imekwenda kwa Thierry Henry na ikisha Gary Neville. Wachambuzi mahiri wa soka katika studio za Sky Sport. Kucheza mpira, kuchambua mpira, ni kitu tofauti kabisa na kufundisha mpira ukiwa umekaa katika benchi.

Roy Keane akiwa kama kocha msaidizi wa Martin O’Neil wamefukuzwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ireland kufuatia matokeo mabaya. Thierry Henry anachapwa kila siku katika kikosi chake cha Monaco. Alijitumbukiza katika kazi hiyo baada ya kuwa msaidizi wa Roberto Martinez katika kikosi cha timu ya taifa ya Ubelgiji.

Usimsahau Neville ambaye alikwenda Valencia na watu wakaamini kwamba huenda angeyahamishia maneno yake ya studio kwa wachezaji wake na kisha Valencia ingeanza kuwa miongoni mwa timu bora Ulaya. Haikuwezekana.

Kukaa juu ya kiti cha studio inaonekana kuwa kazi rahisi. Mara nyingi unazungumza kitu ambacho kimeshatokea. Ni rahisi kujadili makosa. Hata hivyo kuwa kocha ina maana kwamba unatabiri makosa ambayo yanaweza kutokea na unayafuta kabla hayajatokea.

Kazi ya kujadili makosa ambayo hayajatokea na unayafuta haiitaji uwe mchezaji mahiri wa zamani au uwe mchambuzi. Ni kazi tofauti na ngumu sana. hiki ndicho ambacho kinachowatokea kwa sasa akina Roy Keane na Thierry Henry.

Hapo hapo unagundua kwamba kuna wachezaji hawakufikia viwango vya akina Henry na sasa ni makocha mahiri. Mfano wa haraka unakwenda kwa Jose Mourinho. kumbe inawezekana kipaji chake ni uwezo wa kutabiri makosa kabla hayajatokea na kujaribua kuyapatia ufumbuzi.

Kwa sasa Henry na Keane wataendelea kujifunza na kufahamu ugumu ambao makocha mbalimbali wanaupitia katika kazi zao. Sio kazi rahisi sana kama unavyoweza kuichambua ukiwa studio. Kuna wachezaji wa zamani ambao hawakuweza kuzifanya kazi zote mbili hizi.

Diego Maradona amekuwa akifeli kama kocha kila wakati. Mfalme wa soka duniani, Edson Arantes do Nascimento ‘Pele’ hakuweza kazi zote mbili. Hakuweza kuwa mchambuzi wala kocha. Kila anapotabiri kitu kinakwenda fyongo. Aliwahi kutabiri kuwa Afrika itakuwa imechukua kombe la dunia kufikia mwaka 2000. Leo ni miaka 18 baada ya mwaka huo lakini hakuna timu ya Afrika ambayo imewahi kutinga walau nusu fainali ya michuano yenyewe.

 

 

 

 

Advertisement