Pogba ndiye mchezaji bora EPL 2019/20

Muktasari:

Katika mchezo huo Pogba alikosa penalti na hivyo kuwanyima Man United ushindi, baada ya mpira alioupiga kipindi cha pili kuokolewa na mlinda mlango Rui Patricio, ikiwa ni muda mfupi tangu alipomtaka Marcus Rashford amwachie apige.

MANCHESTER, ENGLAND. GARRY Neville buana! Nyota huyu wa zamani wa Manchester United, amesema kiungo mchezaji wa timu hiyo, Paul Pogba ndiye atakayekuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Englanda (EPL), msimu huu.

Neville ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka nchini humo, alisema juzi usiku baada ya Mashetani hao Wekundu wa Old Trafford kutoka sare ya bao 1-1 na Wolvehampton Wanderers katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa mjini humo.

Katika mchezo huo Pogba alikosa penalti na hivyo kuwanyima Man United ushindi, baada ya mpira alioupiga kipindi cha pili kuokolewa na mlinda mlango Rui Patricio, ikiwa ni muda mfupi tangu alipomtaka Marcus Rashford amwachie apige.

Akichambua mchezo huo katika kituo anachofanyia kazi kwa sasa cha Sky Sports, baada ya mechi hiyo, Neville alisema kwamba haoni sababu za Pogba kutonyakua tuzo ya mchezaji bora wa EPL msimu huu kwa kuwa amekamilika katika kila eneo.

Madai hayo yaliyopokelewa kwa mtazamo tofauti na mashabiki wa soka, yamekuja kukiwa na hali ya sintofahamu kuhusu hatima ya mchezaji huyo ambaye bado hajatulia jijini Manchester tangu alipotua klabuni hapo miaka mitatu iliyopita akitokea Juventus, akihusishwa kujiunga na Real Madrid ama kurejea Juventus.