Pogba awaaga wenzake pale Old Trafford

Muktasari:

  • Juventus pia wanataka kumrudisha nyumbani Pogba lakini inadaiwa kwamba Zidane yupo katika nafasi nzuri zaidi ya kumchukua Mfaransa mwenzake huyo baada ya kuahidiwa dau kubwa la uhamisho wa wachezaji na tajiri, Florentino Perez.

MANCHESTER,ENGLAND.MAMBO hayaeleweki Old Trafford. Kumechachamaa. Sahau kuhusu mechi za jana. Hali ya baadaye kuhusu kiungo wao, Paul Pogba imezidi kuingia gizani baada ya kudaiwa kwamba staa huyo amewaaga wachezaji wenzake klabuni hapo.

Kwa mujibu wa habari zilizotokea Ufaransa na kusambaa Ulaya yote jana, inadaiwa kwamba Pogba amewaambia wachezaji wenzake ambao ni marafiki wa karibu kuwa anataka kuondoka klabuni hapo katika dirisha kubwa la uhamisho mwishoni mwa msimu.

Real Madrid inamtaka staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa na kuna habari kwamba Manchester United haitamzuia kuondoka endapo mwenyewe atalazimisha kuhama ili mradi tu timu zifike katika dau lake halisi.

Endapo United itafeli kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao wakati huu wakiwa katika nafasi ngumu, hilo linaweza kuharakisha kuondoka kwa staa huyo waliyemnunua kwa rekodi ya dunia Pauni 85 milioni katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2016.

Juventus pia wanataka kumrudisha nyumbani Pogba lakini inadaiwa kwamba Zidane yupo katika nafasi nzuri zaidi ya kumchukua Mfaransa mwenzake huyo baada ya kuahidiwa dau kubwa la uhamisho wa wachezaji na tajiri, Florentino Perez.

Pogba amekuwa akilaumiwa kwa kiasi kikubwa kwa kiwango chake kinachoyumba mara kwa mara na alicheza ovyo katika pambano dhidi ya Everton Jumapili ambapo United waliadhibiwa 4-0 ugenini Goodson Park huku mwishoni mwa pambano hilo akiomba radhi.

Inadaiwa kwamba mwenyewe anataka kucheza zaidi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku akipendelea zaidi kucheza chini ya Zidane ambaye kabla ya kuondoka na kurudi tena klabuni hapo alishawahi kumtaka staa huyo akacheza Madrid.

Inadaiwa katika msimu wa 2015/16 Zidane alisafiri hadi Italia kwa ajili ya kula chakula cha mchana na Zidane huku akijaribu kumshawishi kutua Santiago Bernabeu lakini dili hilo lilishindikana kutokana na uhusiano mbovu kati ya Perez na wakala wa Pogba, Mino Raiola.

Tayari baadhi ya wachambuzi wametabiri kuwa staa huyo anataka kuondoka klabuni hapo huku staa wa zamani wa Tottenham na timu ya taifa ya England, Jermain Jenas akimpiga kijembee staa huyo pamoja na kipa David de Gea kwamba wanataka kuondoka klabuni hapo.

“Nadhani kuna mchanganyiko wa wachezaji ambao wengine wanataka kuondoka Manchester United na wengine hawana ubora wa kuchezea Manchester United. Hilo ndio tatizo. Katika kikosi cha kwanza cha United nimewaona wengi,” alisema Jenas mara baada ya kumalizika kwa pambano la United na Everton.

“Wachezaji wanaocheza kwa juhudi kubwa ni wale ambao wanashukuru kuwepo Manchester United. Kama wangekuwa na wachezaji zaidi kama hao wasingekuwa wanapata aina hiyo ya matokeo. Lakini wana wachezaji wengi wakubwa ambao wanaamini wanaweza kwenda timu kubwa na bora zaidi.” Aliongeza staa huyo.