Pogba atasumbua sana vigogo usajili ujao

Muktasari:

  • Juventus wakihitaji tena huduma yake huko ikiwa ni miaka mitatu imepita tangu walipomuuza kwa ada ya Euro 110 milioni mwaka 2016 kwa Manchester United

Turin, Italia. Kiungo Paul Pogba anajiandaa kuachana na Manchester United mwishoni mwa msimu huu, ndicho kinachosemwa.

Gazeti la AS limedai kwamba kiungo huyo baada ya kudumu kwa misimu mitatu huko Old Trafford sasa anataka kuondoka kwenda kuendelea na maisha mengine kwingineko.

Supastaa huyo wa Ufaransa hivi karibuni alisema kwamba Real Madrid ni uhamisho wa ndoto zake, kauli ambayo imeibua wasiwasi mkubwa kutoka kwa mashabiki wa Man United wakiwa na hofu kwamba mchezaji wao huyo anaondoka.

Lakini, jambo hilo limewazindua pia waajiri wake wa zamani Pogba, mabingwa wa Italia, Juventus wakihitaji tena huduma yake huko Turin ikiwa ni miaka mitatu imepita tangu walipomuuza kwa ada ya Euro 110 milioni mwaka 2016.

Lakini, wapi Pogba atakwenda itategemea na wakala Mino Raiola, ambaye amekuwa na uhusiano mzuri sana na Juventus kuliko Real Madrid na bosi wao Florentino Perez.

Wiki iliyopita kiungo huyo alisema: "Ni kama ninavyosema siku zote, Real Madrid ni ndoto ya kila mmoja. Ni moja ya klabu kubwa duniani. Pia kuna Zinedine Zidane kama kocha na kucheza chini yake ni ndoto ya kila mmoja anayependa soka. Kwa sasa nipo Manchester, lakini hatuwezi kujua yatakayotokea baadaye. Nikiwa Manchester nina furaha."