MTAA WA KATI : Pogba ataondoka Old Trafford na deni kubwa

Wednesday July 10 2019

 

By Said Pendeza

TUNA makosa. Sote tuna makosa. Tukubali hili. Tulikosea kumkosoa mtu mzima Sir Alex Ferguson. Tulipomkosoa kisa Paul Pogba. Tulipomkosoa alipomwaacha bure kabisa aenda Juventus.

Tulimkosea yule mzee. Yeye alikuwa naye karibu zaidi. Yeye alifahamu kitu kizuri kutoka kwake. Lakini, alifahamu zaidi matatizo yake. Ndiyo maana hakuona shida kumwaachia Pogba, sisi tuliyemwona ni hodari aondoke kwenye kikosi chake burebure.

Ninachoamini kwa sasa Pogba asingerudi Man United kama Ferguson angeendelea kuwapo. Kwa sababu alimfahamu vyema. Sisi tuliamini kwamba Pogba ni kiungo wa goli hadi goli. Tuliamini ni sawa na Patrick Vieira au Roy Keane. Tuliamini ni sawa na Arturo Vidal au Yaya Toure.

Tuliamini hivyo kuwa ni Michael Essien. Tulikosea na hapo ndipo tulipomkosea yule mzee. Pogba ni mtu tofauti kabisa. Ukakamavu wa mwili wake ni tofauti na ambacho unaamini angefanya uwanjani. Pogba hakusaidii kunyang’anya mipira 50 hadi 60 kutoka kwa wapinzani. Si kiungo mwenye mapafu ya kucheza goli hadi goli.

Hana huo uwezo licha ya kuwa na mwili uliojengeka vyema na kuonekana mwenye nguvu. Pogba hataki kuteseka. Pogba wakati anatamba Juventus hadi Man United wakashawishika kumrudisha kikosi kwa pesa nyingi. Kwenye sehemu ya kiungo alikuwa akicheza na Andrea Pirlo, Vidal na wakati mwingine Claudio Marchisio.

Hao walifanya kazi zote za kishetani ndani ya uwanja, Pogba yeye alibaki kuwa huru tu. Alicheza kwa kustarehe. Pogba anakupa matokeo chanya mfumo wa kutumia viungo watatu wa kati.

Advertisement

Akiwa na Timu ya Taifa ya Ufaransa anafanya vyema kwa sababu kunakuwa na N’Golo Kante, Blaise Matuidi, ambao wamekuwa wakifanya vurugu zote za kuifanya mipira iwe kwenye himaya yao.

Hayo ni maisha ambayo hakuyakuta Man United. Mara nyingi amepangwa kwenye safu ya viungo wawili, ameteseka. Hana alichokifanya uwanjani.

Mara chache alizopangwa kwenye safu ya viungo watatu, amejaribu kufurukuta.

Pogba alihitaji Ander Herrera na Nemanja Matic wawepo uwanjani, ili yeye afanye vyema. Kupata huduma bora ya Pogba, lazima uwe na viungo wawili wa kukaba tu.

Hayo maisha hayapo Man United. Ndio maana anataka kuondoka. Real Madrid anakotaka kwenda maisha yatakwenda kuwa mepesi. Atacheza na Casamiro, Toni Kroos na Luka Modric kwenye sehemu ya kiungo. Hakuna atakayekuwa akimtolea sana macho. Macho ya wengi yatakuwa kwa Eden Hazard. Hapo, Pogba atakwenda kuwa bora uwanjani.

Hatopewa majukumu ya kukaba uwanjani. Bila shaka Zidane atakwenda kumtumia kama alivyomtumia Isco kwenye msimu wake wa mwisho wanabeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Alimfanya kuwa huru uwanjani.

Hakuhusika na kazi za kunyang’anya mipira. Kroos, Casemiro na Modric walifanya kazi hiyo. Hivyo ndivyo atakavyokwenda kucheza huko Bernabeu. Old Trafford hayo maisha hayapo. Lakini, pia kila mtu amekuwa akimtazama yeye. Wakiamini kuna kitu anaweza kukifanya.

Hakukifanya na hawana imani naye tena. Hilo ni jambo jingine linalomfanya Pogba atake kuondoka Man United, mashabiki hawaona hawapi kile wanachokihitaji. Msimu uliopita alishindwa kadi kwenye bato na Ruben Neves.

Hakuiweza kabisa bato ya Sergio Busquets. Aliiishindwa hadi bato ya Idrissa Gueye, Man United ilipochapwa Nne Bila na Everton kwenye Ligi Kuu England. Lakini, Real Madrid wanataka kulipa Pauni 120 milioni kunasa saini yake. Kweli Pogba wa Pauni 120 milioni? Au Man United wanavyoomuza Pauni 150 milioni. Kweli Pogba ni wa thamani hiyo? Kiungo asiyetaka shida.

Amerudi Man United kwa pesa nyingi, Pauni 89 milioni. Lakini, anataka kuondoka akiwa hawajawatendea haki mashabiki wake.

Hatakuwa tofauti na Angel Di Maria, siku akirudi Old Trafford ushangae atakapopokewa kwa kelele za kuzomewa na mashabiki. Si kama Cristiano Ronaldo au mastaa wengine ambao hadi leo wakirudi Man United wanafurahiwa.

Pogba halitaka hilo, anaondoka akiwa hajamaliza kiu ya mashabiki wake Old Trafford. Bado ana deni kubwa.

Advertisement