Pogba atamani kukipiga Madrid

Manchester, England. Paul Pogba amebainisha ndoto ya siku moja kuja kuichezea Real Madrid, jambo lililozua mashaka juu ya majaliwa yake ndani ya klabu ya Manchester United.

Kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa, hata hivyo alisisitiza kuwa ana furaha kuwapo Old Trafford kwa sasa, huku pia dirisha la usajili likifungwa Jumatatu iliyopita.

Lakini Pogba ameleta habari hizo akiwa bado haijulikani kama atataka kuendelea kuichezea Man United baada ya mkataba wake wa sasa kumalizika huku akiwa katika majukumu ya timu ya taifa.

Kiungo huyo mwenye miaka 27, alisema: “Nipo na Manchester United kwa sasa. Mnafahamu kwamba jambo hili limekuwa likizungumzwa sana, wakati mimi sikuwahi kulizungumzia.

“Nilisikia kelele nyingi kwamba nilikuwa nataka kuondoka ama naondoka ndani ya klabu yangu ya sasa.

“Leo (jana), mnaniona bado nipo Manchester United na bado napambana kwa ajili ya kuirudisha klabu yangu kileleni zaidi.

“Nyote mmekuwa mashahidi wa jambo hili la mimi kutaka kuondoka. Mnataka kusikia majibu yangu?

“OK, wachezaji wote wangependa kucheza katika klabu ya Real Madrid.

Labda ni ndoto za wachezaji wengi. Hilo pia kwangu ni ndoto, kwanini isiwe hivyo siku moja?

“Kama ambavyo nimetangulia kusema, nina furaha kuwa mchezaji wa Manchester United na naipenda klabu yangu. Najitahidi kuonyesha kiwango ndani ya Man United, nafurahia soka yangu hapo na nataka kufanya kila liwezekanalo kuirudisha klabu kileleni.