Pogba atajuta kisa Madrid

MANCHESTER, ENGLAND. MATUMAINI ya kiungo, Paul Pogba kwenda kujiunga na Real Madrid huenda yakashindwa kutimia baada ya miamba hiyo ya Bernabeu kufikiria mastaa tofauti kabisa katika mpango wao wa kuunda Galacticos mpya.

Mabingwa hao wa La Liga wanatunza pesa yao kwa ajili ya kufanya usajili mkubwa kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwakani, huku wachezaji inaotaka kuwasajili ni Kylian Mbappe, Erling Haaland na kiungo kinda Eduardo Camavinga.

Pogba, 27, hakutaka kuweka siri kuhusu kuhusudi maisha ya kwenda kucheza Bernabeu.

Alhamisi iliyopita alisema: “Ndio, wachezaji wote wangependa kuichezea Real Madrid. Pengine ni ndoto. Ni ndoto kwangu, kwanini isiwe siku moja?”

Lakini, gazeti la AS linaandika Pogba anaweza kubaki kwenye huzuni kubwa. Mbappe anaendelea kubaki kwenye rada za Los Blancos baada ya kuonyesha dhamira ya kuachana na Paris Saint-Germain mwakani wakati huo mkataba wake ukiwa umebaki mwaka mmoja.

Ripoti kutoka Hispania zinadai PSG inaweza kumuuza Mbappe kwa bei ndogo kati ya Pauni 111 milioni na Pauni 91 milioni wakati atakapoingia miezi yake 12 ya mwisho ya mkataba wake huko Paris.

Kiungo kinda Camavinga, 17, anasakwa kwa nguvu zote na Real Madrid huku wakipanga kutumia Pauni 25 milioni kumng’oa kutoka Rennes. Kocha, Zinedine Zidane atapiga hesabu pia za kumnasa, Haaland kwenye majira yajayo ya kiangazi.