Pogba alianzisha upya Man United

Muktasari:

  • Viongozi wa Kambi ya Los Blancos wamekuwa wakimtafuta Pogba na huenda staa huyo wa Ufaransa akashawishika kwa kuwa Zinedine Zidane ndiye kocha wa klabu hiyo kwa sasa.

LONDON, England. Paul Pogba anatarajiwa kuanza mazungumzo ya kuongeza mkataba na klabu ya Manchester United lakini kasi hiyo ya mazungumzo inachagizwa na suala la Real Madrid kumtaka mchezaji huyo.

Viongozi wa Kambi ya Los Blancos wamekuwa wakimtafuta Pogba na huenda staa huyo wa Ufaransa akashawishika kwa kuwa Zinedine Zidane ndiye kocha wa klabu hiyo kwa sasa.

Na katika siku za karibuni nyota wa Manchester United Paul Pogba aliweka wazi kwamba ndoto zake ni kuchezea kikosi cha Real Madrid siku moja na suala la kudai Pauni 500,000 kwa wiki kama mshahara linaonekana kama ni mbinu ya kutaka kuondoka kambi ya Old Trafford.  

“Kama ambavyo nimekuwa nikisema mara kwa mara kwamba Real Madrid ni klabu kubwa na ni ndoto ya kila mchezaji kuchezea klabu hiyo,” alisema Pogba.

“Kinachovutia zaidi ni kuwa [Zinedine] Zidane ndio kocha. Hakuna mchezaji ambaye hapendi kufundishwa na mtu kama huyo mwenye historia kubwa na mafanikio katika mchezo huu.”

“Lakini kwa sasa bado nipo Manchester United. Hata hivyo huwezi kutabiri au kusema juu ya maisha ya baadae. Bado nina furaha katika kikosi cha United kwa sasa.”

Habari kutoka Real zinasema kwamba klabu hiyo ipo tayari kutoa Pauni 125 milioni kwa ajili ya kumnasa  Pogba katika dirisha la usajili linalokuja. Hata hivyo Kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer wiki iliyopita alisema kuwa mchezaji huyo haendi kokote.

Na katika harakati za kuhakikisha mchezaji huyo anabaki Manchester United wameanza mazungumzo na Pogba, ambaye hata hivyo anataka mshahara wa Paini 500,000 kwa wiki ili abaki.

Mkataba wa Pogba wa sasa katika klabu hiyo umebakiza miaka miwili kabla ya kumalizika na viongozi wanataka kumungezea miezi mingine 12.