Pogba United wanasema imeisha hiyoo

MANCHESTER, ENGLAND. VIJANA wa mjini wanasema imeisha hiyooo. Ndio, kiungo wa Manchester United, Paul Pogba amefuta mpango wa kuachana na wababe hao wa Old Trafford.

Pogba, ambaye amekuwa akiwindwa kwa muda mrefu na Real Madrid na Juventus, amefunguka kuwa anataka kuendelea kubaki Old Trafford na kwamba, ubora wa kikosi hicho umekuwa ukimpa mzuka zaidi.

Pia, amesema kutua kwa kiungo Bruno Fernandez kumetoa mchango mkubwa kwenye kikosi cha Kocha Ole Gunnar Solskjaer, na anafurahia kucheza sambamba na Mreno huyo.

Kutokana na hilo, Pogba amesema kwa sasa yupo tayari kuanzisha mazungumzo kwa ajili ya mkataba mpya ili kuendelea kukipiga kwa muda mrefu huko Old Trafford.

Pogba, ambaye mkataba wake wa sasa umebakiza mwaka mmoja kukiwa na kipengele kinachoipa United nafasi ya kumuongezea mwaka mmoja zaidi, huku Solskjaer akifichua juzi kuwa Mfaransa huyo atakuwepo katika kikosi hicho kwa muda mrefu.

Awali, kulikuwa na mvutano mkubwa baina ya mabosi wa Man United na wakala wa Pogba, Mino Raiola ambaye alikaririwa akisema kuwa mteja wake hana furaha na kikosi cha United na anafikiria kumtafutia makazi mapya.

Hata hivyo, imebainika kuwa Pogba aliyenaswa kwa dau la pauni 89 milioni mwaka 2016 anafurahia kucheza sambamba na Bruno ambaye ujio wake umeifanya Man United kuimarika zaidi na kuifanya kupata matokeo mazuri tofauti na mambo yalivyokuwa awali.

Kombinesheni ya Bruno na Pogba imeifanya Man United kuwa moto kwelikweli ikicheza mechi 16 bila kupoteza huku ikipiga soka la kuvutia na kuonyesha mwanga wa kurejea kwa kikosi kama kile cha enzi za Sir Alex Ferguson.

Hata hivyo, Man United watalazimika kumtengea Pogba mshahara wa maana zaidi ya anaolipwa sasa wa Pauni 290,000 kwa wiki na bonasi nyingine kibao.

Tayari Solskjaer amefichua kuwa Nemanja Matic na Scott McTominay wamesaini mikataba mipya ya kuendelea kukipiga Old Trafford.

“Natambua tangu Pogba amerejea baada ya kupona majeraha amekuwa kwenye kiwango bora na atazidi kuwa bora zaidi. Kwa sasa anafurahia kucheza soka la kiwango chake, tutaona atatupeleka wapi wakati huu tukiwa kwenye vita ya kuwania nafasi nne za juu,” alisema Solskjaer.

Wakati Pogba akitoa habari njema kwa mashabiki wa Man United, mabosi wa klabu hiyo wako kwenye harakati ya kuongeza mastaa wapya huku majina ya nahodha wa Aston Villa, Jack Grealish na winga wa Borussia Dortmund, Jadon Sancho yakiwa kwenye rada.