Pogba, Aubameyang kimenuka!

Muktasari:

  • Kasi ya Man United kwa sasa inatisha. Wameshinda mechi zao tano mfululizo zilizopita, ikiwamo moja dhidi ya wababe waliopo kwenye Top Four, Tottenham. Kwa hali ilivyo, baada ya mechi tano zijazo kwa kila timu, kila kitu kitakuwa kimejiweka bayana kwenye vita hiyo ya kuwania kuwamo ndani ya Top Four.

LONDON, ENGLAND.UNAUSOMA msimamo wa Ligi Kuu England msimu huu ulivyo? Pale kwenye Top Six kuna tofauti ya pointi 16. Liverpool wanaoongoza na pointi zao 57 na Manchester United ndio wanaoshika nafasi ya sita na pointi zao 41. Pointi hizo wamelingana na Arsenal waliopo kwenye nafasi ya tano.

Kwa maana hiyo, Arsenal na Man United zimetofauti kwa mabao mawili tu. Manchester City wao wapo kwenye nafasi ya pili na pointi zao 53, nne nyuma ya vinara Liverpool. Tottenham Hotspur wapo kwenye nafasi ya tatu wakiwa na pointi 48, moja zaidi ya Chelsea waliopo kwenye nafasi ya nne.

Hapo ndipo kwenye utamu halisi. Ligi Kuu England ilipofika kwa sasa, Top Four imekuwa na mvuto zaidi na sasa ni kazi kwa mastaa kama Paul Pogba, Pierre-Emerick Aubameyang, Harry Kane na Eden Hazard kuzibeba timu zao kwenye mchakamchaka huo wa kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Kasi ya Man United kwa sasa inatisha. Wameshinda mechi zao tano mfululizo zilizopita, ikiwamo moja dhidi ya wababe waliopo kwenye Top Four, Tottenham. Kwa hali ilivyo, baada ya mechi tano zijazo kwa kila timu, kila kitu kitakuwa kimejiweka bayana kwenye vita hiyo ya kuwania kuwamo ndani ya Top Four.

Man United wao wanaonekana kuwa na ratiba nyepesi kwenye mechi zao tano zijazo kwenye ligi, ambapo kwanza watacheza na Brighton na Burnley uwanjani Old Trafford, kisha itatoka kuwafuata Leicester City na Fulham halafu itarudi tena nyumbani kuwakabili Liverpool. Kimsingi, mechi ngumu kwa Man United nni hiyo ya kuwakabili Liverpool Old Trafford.

Arsenal wao mambo yao ni magumu na kwenye hili hakika inahitaji msaada mkubwa kutoka kwa mastaa wake kama Aubameyang na Alexandre Lacazette. Mechi ijayo, kwanza Arsenal wataanza na Chelsea uwanjani Emirates, kabla ya kuwakaribisha Cardiff City uwanjani hapo na kutoka kwenye Etihad kuvaana na Man City na kumalizia tena ugenini kwa Huddersfield.

Hakika, Arsenal anaonekana kuwa na ratiba ngumu kwenye mechi zake hizo tano zijazo kwenye ligi. Chelsea wao wanaotegemea zaidi ubora wa Hazard kufunga mabao yake, mechi zao tano zijazo, wataanza na Arsenal huko Emirates, kisha watarudi Stamford Bridge kuwakabili Tottenham. Baada ya hapo watatoka kwenda kuwakabili Bournemouth kabla ya kurudi nyumbani kucheza na Huddersfield na kisha kutoka tena kwenda Etihad kucheza na Man City. Hakika Maurizio Sarri anakabiliwa na ratiba ngumu kwelikweli kwenye mchakamchaka huo wa kuifukuzia Top Four yenye tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Tottenham ambao hawatakuwa na huduma ya straika wao namba moja, Kane, anayetarajia kurudi uwanjani mwanzoni mwa Machi baada ya kuumia, yenyewe kwenye mechi zijazo, wataanza kwa kumenyana na Fulham ugenini, kisha watarudi Wembley kukipiga na Watford. Baada ya hapo watacheza na Newcastle kwenye uwanja huo huo na kufuatiwa na mechi dhidi ya Leicester City kabla ya kutoa kuwafuata Burnley.

Ratiba ngumu sana kwa kocha Mauricio Pochettino, lakini shida ni kwamba hatakuwa na fowadi wake huyo namba moja na yule mwingine, Hueng-Min Son, ambaye kwa sasa yupo na kikosi cha Korea Kusini huko kwenye michuano ya Kombe la Asia. Hivyo ndivyo ilivyo taswira ya mechi hizo tano zijazo za vigogo hao wanne ambao kimsingi ndio wanaowania nafasi mbili za kutinga kwenye Top Four.