Pochettino kafyumu, kisa wachezaji vimeo

Muktasari:

  • Kwa hasira, Pochettino alisema: “Ni vigumu sana kuwaelewa hawa wachezaji kwa jinsi walivyoanza kucheza kipindi cha pili na kuwapa nafasi Southampton kuweza kutawala mchezo na kupata ushindi huo ambao haukutarajiwa.

LONDON, ENGLAND. MAURICIO Pochettino amewachenjia wachezaji wake akiwaambia hovyo kabisa baada ya kukubali kichapo kutoka kwa Southampton kwenye Ligi Kuu England juzi Jumamosi.

Kocha huyo wa Tottenham Hotspur, Pochettino amekiri kiwango cha timu yake kwa sasa kimeanza kumtia wasiwasi na huenda wakashindwa kumaliza ndani ya Top Four kwenye ligi hiyo msimu huu.

Spurs ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa straika wake, Harry Kane lakini Southampton, ambayo ni timu ya zamani ya Pochettino ilisawazisha kupitia kwa Yan Valery kabla ya James Ward-Prowse kuweka msumari wa pili kwa mpira wa adhabu aliopiga kutoka umbali wa mita 25.

Kwa hasira, Pochettino alisema: “Ni vigumu sana kuwaelewa hawa wachezaji kwa jinsi walivyoanza kucheza kipindi cha pili na kuwapa nafasi Southampton kuweza kutawala mchezo na kupata ushindi huo ambao haukutarajiwa.

“Sijui kwanini wamebadilisha staili yatu tuliyokuwa tukicheza. Ni ujinga tu. Hili ni kosa letu, tunapaswa kulaumiana kwa makosa haya.”

Kichapo hicho kimeifanya Spurs sasa kujiweka kwenye nafasi ngumu na kusogelewa na vigogo wengine walipo nyuma yake kama Manchester United na Arsenal, ambazo usiku wa jana zilitarajiwa kumenyana \huko Emirates.

Kabla ya mechi hiyo ya Emirates, Spurs ilikuwa imeizidi Manchester United pointi tano tu, ikiizidi Arsenal pointi sita, hivyo yoyote atakayekuwa ameshinda kwenye mechi hiyo basi atapunguza pengo la pointi lililopo ama kubaki kuwa mbili au tatu.

Kama mchezo huo ukimalizika kwa sare Spurs itakuwa inapumua kwa sababu pengo la pointi litakuwa limebaki pointi nne kwenye hiyo nafasi ya tatu.