Pochettino Man United ataisikia redioni tu

Muktasari:

Hata hivyo, Pochettino anawindwa na klabu nyingine kubwa za Ulaya ikiwamo mahasimu wa Spurs ambao nni Arsenal na Everton, huku Bayern Munich wakiripotiwa kujitoa kwenye mbio za kumtaka kocha huyo. Kuhusu Man United miaka ya karibuni walikuwa wakitamani sana kumvuta kocha huyo kwenye kikosi chao huko Old Trafford baada ya kupendezwa na kazi yake aliyokuwa akifanya Spurs.

MANCHESTER, ENGLAND . MATUMAINI ya Mauricio Pochettino kwenda kuwa kocha mpya wa Manchester United yanazidi kufifia siku baada ya siku.
Muargentina huyo kwa sasa hana kazi baada ya kupigwa chini ya Tottenham Hotspur mwezi uliopita na jina lake lilikuwa likitajwa sana huko Old Trafford kwamba angeenda kuchukua mikoba ya Ole Gunnar Solskjaer.
Hata hivyo, Pochettino anawindwa na klabu nyingine kubwa za Ulaya ikiwamo mahasimu wa Spurs ambao nni Arsenal na Everton, huku Bayern Munich wakiripotiwa kujitoa kwenye mbio za kumtaka kocha huyo. Kuhusu Man United miaka ya karibuni walikuwa wakitamani sana kumvuta kocha huyo kwenye kikosi chao huko Old Trafford baada ya kupendezwa na kazi yake aliyokuwa akifanya Spurs.
Lakini, kocha Solskjaer amezinduka upya kabisa kwennye kikosi cha Man United, kikitoa tu vichapo jambo lililobadili akili za mabosi wakubwa kwenye timu hiyo ambao sasa wamemua kutulizana na kocha huyo. Ushindi wa kibabe kabisa dhidi ya  Spurs, Manchester City na AZ Alkmaar, Man United ikishinda mabao manane katika mechi hizo na kufungwa mawili tu, yamepagawisha mabosi na sasa wala hawataki kusikia kitu kinachoitwa Pochettino. Na sasa mpango uliopo ni kumsapoti kocha wao katika kumletea wachezaji wapya kwenye dirisha la Januari baada ya kuifikisha timu kwenye nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu England huku ikifuzu hatua inayofuata ya michuano ya Europa League tena kwa kuongoza kundi lao. Kutokana na hilo, haieleweki kama Pochettino ataendelea kusubiri Solskjaer akwame au ataamua kuchukua dili la timu nyingine tu akapige kazi. Man United kwenye nafasi ya tano wanayoshika kwenye ligi, wapo pointi tano tu nyuma ya timu inayoshika namba nne, Chelsea ya Frank Lampard na kesho Jumapili watakipiga na Everton uwanjani Old Trafford.