Pochettino, Manchester United wapo mezani

Muktasari:

Iliaminika pia angeenda kuchukua mikoba ya kuinoa Manchester United wakati Jose Mourinho alipofutwa kazi Desemba 2018, lakini wababe hao wa Manchester waliamua kumchukua jumla Solskjaer baada ya kuwaonyesha kiwango bora kwenye mechi zake za kwanza alipokuwa kocha wa muda.

Manchester, England. Lisemwalo ni kwamba Mauricio Pochettino yupo kwenye mazungumzo na mabosi wa Manchester United kwa ajili ya kwenda kumbadili kocha Ole Gunnar Solskjaer huko Old Trafford.

Muargentina huyo amekuwa akihusishwa na kwenda kukalia kiti cha moto huko Old Trafford baada ya kufutwa kazi Tottenham Hotspur, Novemba mwaka jana.

Iliaminika pia angeenda kuchukua mikoba ya kuinoa Manchester United wakati Jose Mourinho alipofutwa kazi Desemba 2018, lakini wababe hao wa Manchester waliamua kumchukua jumla Solskjaer baada ya kuwaonyesha kiwango bora kwenye mechi zake za kwanza alipokuwa kocha wa muda.

Lakini, sasa mabosi wa Man United wanafikiria kufanya uamuzi sahihi baada ya timu kutokuwa na matokeo yanayoeleweka. Taarifa za kutoka Italia zinadai kwamba Man United wameshaanza mazungumzo na Pochettino, ambaye pia yupo tayari kwenda kupiga mzigo huko Old Trafford.

Man United ya Solskjaer imekuwa haeleweki kiwango chake cha uwanjani na jambo hilo ndilo linalodaiwa kuwafanya mabosi wa miamba hiyo kufikiria kumleta mtu atakayekuja kuleta mambo matamu.

Kocha mwingine anayedaiwa kwamba anaweza kufikiriwa kwa haraka kwenda kumbadili Solskjaer ni Mtaliano, Max Allegri.