Pluijm akitolea macho kibarua cha kuinoa Taifa Stars

Muktasari:

Mholanzi huyo amefundisha kwa mafanikio katika klabu za Yanga, Singida United na Azam kwa nyakati tofauti

Dar es Salaam. Kocha wa zamani wa Yanga na Azam, Hans van Pluijm amekimezea mate kibarua cha kuinoa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ baada ya kutimuliwa kwa Emmanuel Amunike.

Amunike alitimuliwa siku chache zilizopita baada ya kufanya vibaya kwa Taifa Stars katika fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON’ nchini Misri zinazoendelea kutimua vumbi.

Pluijm alisema akionekana anasifa za kuwa mrithi wa Amunike milango ipo wazi na atakuwa tayari kurejea nchini kuchukua mikoba ya Mnigeria huyo.

Kocha huyo wa Kiholanzi, alisema anauzoefu wa kutosha kutokana na kuzifundisha klabu kadhaa za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mafanikio, ikiwemo Yaanga na Singida United na Azam.

“Wenye uamuzi ni TFF kama wakiona ninafaa basi naweza kuwa msaada wa kuivusha timu ya taifa ya Tanzania ilipo kwa kupiga hatua, ni muda wa kujaribu kuwa na misingi ya mpira ambayo itakuwa ikiendelezwa.

“Hakuna kitu kibaya kama kutokuwa na msingi nachojua ikiwepo hata kocha akiondoka basi ni lazima anayekuja aje na mipango yake itakayokuwa ikifuata misingi iliyopo,” alisema.

Klabu ya mwisho, Pluijm kuifundisha nchini kabla ya kurejea kwao ilikuwa Azam ambayo aliipa mafanikio ya kutwaa ubingwa wa kombe la Mapinduzi.

Kocha huyo, amekuwa akitumia mbinu za kucheza soka la kushambulia kwenye ufundishaji wake huku akiwatumia viungo wakabaji wenye uwezo wa kusambaza mipira kwa haraka.