Pluijm, Mwambusi watimuliwa Azam FC

Muktasari:

Taarifa iliyotolewa awali inaeleza kuwa msaidizi wa Mholanzi huyo, Juma Mwambusi naye ametimuliwa.

Dar es Salaam. Kipigo cha mabao 3-1 cha Azam FC kutoka kwa Simba jana Ijumaa katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kimemfungisha virago Mholanzi Hans van der Pluijm mwenyewe amethibisha akisema hana presha.

Pluijm ametimuliwa leo Jumamosi baada ya kufanyika kikao kizito na vigogo wa Azam FC, alisema siku zote kazi ya ukocha haina dhamana unaajiriwa ili ufukuzwe hivyo anajiandaa kuanza maisha mapya sehemu nyingine.

“Namtakiwa mafanikio mema kocha ajaye, nimekuwa na wakati mzuri Azam FC na nilijitahidi kadri niwezavyo ili kufikia malengo ya klabu lakini ndiyo hivyo, naamini atakayekuja ataendeleza kile nilichofanya,”alisema Pluijm kocha mwenye uzoefu na soka la Afrika baada ya kufanya kazi kwa kipindi kirefu nchini Ghana kabla ya kuja nchini na kujiunga na Yanga baadaye Singida United na Azam FC aliyomalizana nayo leo

“Nawatakiwa mafanikio mema kwa siku chache za usoni Klabu ya Azam kwani wanaweza kutawala soka la Tanzania maana wamejipambanua kwa kuwa na miundo mbinu mingi ya kisasa.”

Kocha huyo aliendelea mbele na kusema: “Asanteni mashabiki wa Azam FC ambao siku zote hata kwenye kipindi kigumu mlikuwa nyuma yangu mkinisapoti.”

Taarifa iliyotolewa awali inaeleza kuwa msaidizi wa Mholanzi huyo, Juma Mwambusi naye ametimuliwa. Makocha hao walianza kuinoa Azam FC mwanzoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara.