Pluijm, Edo walichambua bao la Samatta

Muktasari:

Samatta anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kucheza na kufunga bao katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

KOCHA wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm na mchambuzi, Edo Kumwembe wamelichambua bao la nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Mbwana Samatta dhidi ya Liverpool ambalo limepigiwa kura na kuwa bao bora la mwaka la KRC Genk.

Mei 25, klabu ya KRC Genk kupitia ukurasa wao rasmi wa Instagram, walitangaza kuwa mshindi wa goli bora la mwaka ni  Samatta ambaye alikuwa akiichezea timu hiyo kabla ya Januari mwaka huu  kujiunga na Aston Villa ya England.

Pluijm alisema  haikuwa kazi nyepesi kwa Samatta kufanya anachotaka mbele ya mabeki bora kabisa duniani, "Ile mechi nilipata nafasi ya kuitazama, lilikuwa bao bora kabisa kumuona akifunga Samatta, ni kama aliruka na kuganda juu akisuburi mpira. Ilikuwa maridadi kabisa."

Upande wake Edo ambaye amekuwa akimtembelea mara kwa mara Samatta tangu akiwa DR Congo hadi Ubelgiji, alisema kwa Genk kupata bao tena Anfield halikuwa jambo la kawaida, inaweza kuwachukua muda.

"Sam alifunga mbele ya mabeki bora tena katika uwanja mgumu wa Anfield, kuna timu kibao zimeshindwa kupata mabao pale lakini tukumbuke kuwa timu aliyokuwa akiichezea sio timu kubwa kihivyo Ulaya," alisema.

Novemba 5, 2019, Samatta alifunga bao hilo ambalo limepigiwa kura na kushinda bao bora la mwaka  kwenye uwanja wa Anfield ikiwa ni mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool.

Ilikuwa ni dakika ya 41 kipindi cha kwanza, kichwa kikali cha Samatta kikaipa Genk goli la kusawazisha  lakini mwisho wa mchezo Liverpool iliibuka na ushindi wa mabao  2-1.

Katika kinyang'anyiro hicho cha bao bora la mwaka la KRC Genk,  Samatta alikuwa akishindanishwa na mabao ya Hagi, Berge, Maehle, Thorstvedt, Hroŝovský na Ito.