Pira gwaride lazua balaa zito

KUUMIA kwa straika Chris Mugalu saa chache kabla ya kupigwa kwa pambano la Simba dhidi ya Tanzania Prisons jana mkoani Rukwa, kumemtibulia Kocha Sven Vandanbroeck aliyemtegemea nyota huyo kutoka DR Congo kuliamsha dude mbele ya maafande hao waliopata ushindi wa bao 1-0.

Kipigo hicho kimemuibua, muwezeshaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ na Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzales ambao waliwasisitiza mashabiki kuganga yajayo na kutovunjika moyo kwani kilichotokea ni sehemu ya mchezo na kisiwatoe kwenye ushindani.

Ushindi huo wa Prisons, umetibua rekodi ya Simba ambao walikuwa hawajapoteza mchezo wowote katika Ligi Kuu Bara tangu walipofungwa mabao 3-2 na Mbao FC kwenye mechi ya msimu uliopita uliopigwa Julai 16.

Simba imekumbana na kipigo cha kwanza msimu huu na kujikuta ikiporomoka kutoka nafasi ya pili hadi ya tatu ikibaki na pointi zao 13 kutokana na mechi sita, ilijikuta ikicheza mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, huku pengo la wazi la kukosekana kwa kina Meddie Kagere, John Bocco, Clatous Chama na Mugalu likionekana.

Kagere na Bocco waliachwa Dar kutokana na kuwa majeruhi, huku Chama akiwa ameenda kwao Zambia, na Mugalu aliumia akijiandaa na mchezo huo na kumlazimisha Sven kumuanzisha Charles Ilanfya ambaye hakuwa na maajabu na hata alipoingia Miraj Athuman hakubadili chochote.

Mugalu mwenye mabao matatu aliumia mazoezini na kuvuruga mipango ya Sven dhidi ya Prisons ambao walipata ushindi wao wa kwanza mbele ya Simba tangu msimu wa 2016-2017 ikiwa nyumbani.

Dalili za Simba kupoteza mchezo zilianza mapema baada ya kuumia kwa Shomari Kapombe dakika ya 14 tu ya mchezo baada ya kugongana na Joash Onyango wakati wakiwa kwenye harakati za kuokoa mpira langoni mwao na kumfanya Sven amuingize Kennedy Juma aliyebadilishana nafasi na Erasto Nyoni aliyecheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu chini ya kocha huyo Mbelgiji.

Bao la kichwa la dakika ya 48 lililofungwa na Samson Mbangula liliwafanya wachezaji wa Prisons kushangilia kwa staili ya wimbo huo ‘Fimbu’ wa mkali Felix Wazekwa wa DRC ikionyesha ishara ya kuchapa fimbo.

Salum Kimenya ndiye aliayenzisha mpira wa kurusha kwa Ismail ambaye naye alipiga krosi kwa Mbangula aliyeruka zaidi ya beki Onyango na kupiga kichwa kilichoupeleka mpira wavuni na kumuacha kipa wa Simba, Aishi Manula akiingia katika lawama kutokana na kufanya hesabu mbovu za kutoka mbele kidogo ya lango wakati krosi ikipigwa kuelekea kwa mfungaji, na alipotaka kurudi golini akachelewa na kuushuhudia mpira ukiwa ndani ya nyavu.

Prisons licha ya uchovu wa kucheza mechi mbili ndani ya siku tatu katika mikoa tofauti, ilicheza kwa kiwango bora zaidi ya mabingwa.

Mfungaji wa bao la Prisons, Mbangula alisema hakuna kitu kilichowasaidia kupata ushindi huo zaidi ya wachezaji wote kujitoa na kupambana sana, huku nahodha wake Benjamini Asukile akisema pira Gwaride ndilo limewamaliza Simba.

“Hatukuwakamia Simba ili tuliwakabili kwa kuwaheshimu kwa sababu tunajua uwezo wao ni mkubwa ila tuliingia kwa kujiamini kutokana na mipango ya kocha wetu lakini pia tulikuwa bora leo (jana) zaidi yao,” alisema Asukile.

Naye nahodha wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alisema wanakubali matokeo kwani wapinzani wao walikuwa bora uwanjani na hakutaka kutumia sababu ya kuwakosa baadhi ya mastaa wao kama kisingizio.

Simba ilitegemea mashambulizi yaliyoanzishwa na Luis Miquissone na Morrison ambaye kuna wakati alikuwa akijiangusha ovyo uwanjani kulazimisha faida kwa timu yake, japo mwamuzi Shomary Lawi alikuwa akipeta baada ya kubaini ilikuwa janja yake tu.

VIKOSI

Prisons: Jeremiah Kisubi, Michael Ismail, Benjamini Asukile, Vedastus Mwihabi, Nurdin Chona, Jumanne Elifadhil, Salum Kimenya, Ezekia Mwashilindi, Samson Mbangula, Jeremia Juma na Lambart Sabiyanka.

Simba: Manula, Kapombe, Mohammed Hussein, Onyango, Erasto Nyoni, Mkude, Hassan Dilunga, Lally Bwalya, Ilanfya, Luis Miquissone na Morrison.