Pigo Harambee Stars: Olunga kuikosa Ghana, Were ndani

Muktasari:

  • Kuziba pengo la Olunga, Migne amesalimu amri na kumuangukia Straika hatari wa Zesco United, Jesse Were aliyekuwa ameachwa nje ya kikosi cha wachezaji 24, kilichoteuliwa awali.

Nairobi, Kenya. Timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars, imepata pigo baada ya kubainika kuwa Straika wake matata, anayekipiga katika klabu ya Kashiwa Reysol ya Japan, Michael Olunga atakosa mchezo wao dhidi ya Ghana.

Kwa mujibu wa Kocha mkuu wa Stars, Sebastien Migne, Olunga aliumia akiwa na klabu yake ameondolewa katika kikosi kitakachowavaa Black Stars, katika mchezo wa marudiano wa Kundi D.

Stars na Ghana, zitajitosa uwanjani siku ya Jumapili, Machi 23, kwa ajili ya mechi ya mwisho ya kusaka nafasi ya kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2019), ambayo imepangwa kufanyika mjini Kumasi, Ghana.

Kuziba pengo la Olunga, Migne amesalimu amri na kumuangukia Straika hatari wa Zesco United, Jesse Were, ambaye awali aliachwa nje ya kikosi cha wachezaji 24, kilichoteuliwa na Mfaransa huyo.

Kenya wanasafiri kuelekea Ghana, wakiwa kifua mbele, baada ya kushinda mechi ya kwanza, iliyopigwa ugani Moi Kasarani, kwa mabao 2-1. Stars tayari wameshafuzu kushiriki makala ya 32 ya AFCON, yatakayofanyika nchini Egypt, kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.

Stars, leo imepata mdhamini mpya, kampuni ya kubeti ya Betin, iliyoisaini dili la mwaka mmoja la Shilingi 20 Milioni, kwa sasa kinaongoza kundi D, ikiwa na pointi saba, tatu mbele ya Ghana, inayoshika nafasi ya pili.