Pesa zawaponza mastaa wa Simba

Tuesday February 12 2019

 

By Mwanahiba Richard

IMEELEZWA nyota wanaosajiliwa Simba wakitokea timu zenye uwezo mdogo kifedha hushuka viwango baada ya kuendekeza starehe kutokana na matumizi mabaya ya fedha wanazolipwa wakati wa usajili.

Simba ni moja kati ya klabu inayolipa fedha nyingi kwa wachezaji wanaowasajili ambapo mchezaji wa kima cha chini hulipwa Sh 10 milioni naye ni yule aliyepandishwa kutoka timu yao ya vijana lakini usajili wao huanzia Sh 20 milioni.

Baadhi ya wachezaji ndani ya Simba wameshindwa kuonyesha viwango kwasababu mbili kukosa namba kutokana na ushindani kwenye nafasi zao pamoja na starehe.

Wakati wa dirisha dogo la usajili baadhi ya wachezaji walitolewa kwa mkopo ndani ya Simba ambao ni Mohamed Rashid (KMC), Marcel Kaheza (KCB ya Kenya) na Said Mohamed Nduda (Ndanda)

Kaheza na Mo Rashid walishindwa kupambania namba mbele ya John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi wakati Nduda alishindwa kumkalisha Aishi Manula huku akiletewa mpinzani mwingine, Deogratius Munishi ‘Dida’ ambaye ni kipa namba mbili.

Kocha wa makipa wa Mtibwa Sugar, Patrick Mwangata alielezea hilo ugeni wa kushika pesa kwa wakati mmoja ndiyo sababu ya baadhi ya nyota wa Simba kujiingiza kwenye starehe na kusahau majukumu yao ndani ya klabu.

“Simba inalipa vizuri sana wachezaji wao wakati wa usajili lakini zinafika kwenye mikono ambayo ilikuwa na kiu ya muda mrefu kushika pesa nyingi,” alisema Mwangata.

Mwangata alisema endapo Nduda atatulia na kufanyakazi basi alikokwenda ni sehemu sahihi kwake.

“Hebu chukulia tu mfano wa Nduda, ni kipa mzuri sana lakini vitu vichache sana vinamuangusha ambapo anashindwa kutenganisha muda wa kazi na starehe, ameenda Ndanda huko naamini atafanya vizuri kwani ni mzuri na ana vitu vya tofauti,” alisema.

Advertisement