Pepe aahidi taji la Ulaya Arsenal

Muktasari:

Pepe amesaini mkataba wa miaka mitano kwenye kikosi cha Emirates na kuamini kwamba, kazi yake ya kwanza ni kumaliza ukame wa ubingwa wa Ulaya na hilo litaanza kwenye msimu huu huko kwenye Europa League.

LONDON, ENGLAND. STAA ghali zaidi kwenye kikosi cha Arsenal, Nicolas Pepe amesema ametua kwenye timu hiyo kumaliza ukame wa mataji na msimu huu wataanza na ubingwa wa Europe League.

Winga huyo wa kimataifa wa Ivory Coast ametua Arsenal kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi kwa ada ya Pauni 72 milioni na ameahidi kuleta ubingwa wa Ulaya kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Mhispaniola, Unai Emery.

Pepe amesaini mkataba wa miaka mitano kwenye kikosi cha Emirates na kuamini kwamba, kazi yake ya kwanza ni kumaliza ukame wa ubingwa wa Ulaya na hilo litaanza kwenye msimu huu huko kwenye Europa League.

Kwenye mechi mbili alizocheza kwenye kikosi cha Arsenal hadi sasa, ametumikia kwa dakika 63 tu, lakini mashabiki wa timu hiyo wanaamini mkali huyo ataanza kuwasha moto ni suala la muda tu ili kuzoea mazingira.

“Nimechagua kuja hapa kwa sababu klabu hii ina mambo mengi mazuri. Mpango ni kushinda ubingwa Europa League na kufanya vizuri kuliko msimu uliopita. Naamini tutafanya hivyo kwa sababu kila mtu ana kiu,” alisema.

Arsenal ilifika fainali ya Europa msimu uliopita, wakafungwa 4-1 dhidi ya Chelsea huko mjini Baku. Mwishoni wa mwezi huu watafahamu wamepangwa na nani kwenye kundi la michuano hiyo.