Pep kavurugwa! Ajiandaa kutumia Pauni 390mil kusajili mabeki

MANCHESTER ENGLAND. UKUTA wa zege. Pep Guardiola anajiandaa kutumia mkwanja mrefu, Pauni 390 milioni kwenye usajili wa mabeki peke yake.

Dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, beki wa kati wa kimataifa wa Ureno, Ruben Dias, anayekipiga huko Benfica anatarajia kutua Manchester kwenda kukamilisha uhamisho wake wa kujiunga na miamba ya Etihad kwa ada ya uhamisho ya Pauni 64.5 milioni.

Benfica ilitangaza usiku wa Jumapili iliyopita uhamisho huo umeshakubaliwa kila kitu, hivyo kilichokuwa kimebaki ni ishu ya makubaliano binafsi pamoja na kupima vipimo vya afya.

Uhamisho huo utamshuhudia Nicolas Otamendi akitimkia Benfica kwa ada ya Pauni 13.7 milioni baada ya klabu hizo mbili kukubaliana.

Hata hivyo, makubaliano hayo ya kubadilishana wachezaji bado yataigharimu Man United mkwanja wa zaidi ya Pauni 50 milioni kunasa beki kwenye uwezo mkubwa wa kukaba ili kuwarudisha kwenye makali yao ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England. Kwa kile kilichowakuta Man City kwenye mchezo dhidi ya Leicester City, Dias anasubiriwa kwa hamu kubwa huko Etihad.

Licha ya kwamba Vincent Kompany alikuwa akisumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara kwenye miaka yake michache ya mwishoni kwenye klabu hiyo, bado ameacha pengo ambalo limeshindwa kuzibwa tangu alipoondoka Mei 2019. Kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, Man City itakuwa imetumia zaidi ya Pauni 105 milioni kunasa mabeki wa kati pekee, Dias na Nathan Ake.

Kutumia pesa ndefu kwenye usajili wa mabeki huko Man City si kitu kipya kwa Guardiola. Mtangulizi wake, Manuel Pellegrini pesa kubwa aliyotumia kwenye beki ni ile Pauni 30 milioni alizolipa kupata huduma za Otamendi na Eliaquim Mangala kwa kila mmoja. Hata hivyo, bado inaonekana ni ngumu kuamini kama ujio wa Dias utamaliza tatizo la mabeki kwenye kikosi hicho cha Etihad.

Usajili wa mabeki wa kati ambao wamesajiliwa na Guardiola Man City na kumgharimu Pauni 390 milioni ni hawa hapa, John Stones huduma yake ya kutoka Everton aliinasa kwa Pauni 47 milioni. Alilipa Pauni 45 milioni Tottenham Hotspur kumsajili Kyle Walker.

Beki Danilo alimgharimu Pauni 26.5 milioni alipomnasa kutoka Real Madrid, wakati Aymeric Laporte alimnasa kutoka Athletic Bilbao kwa mkwanja wa Pauni 57 milioni.

Guardiola alitumia pesa nyingi kumsajili Benjamin Mendy kutoka AS Monaco kwa Pauni 49 milioni, huku Joao Cancelo, aliyemsajili kutoka Juventus saini yake imemgharimu Pauni 60 milioni. Ake amemsajili kwa Pauni 41 milioni na Dias ndiyo hivyo, Pauni 64 milioni kumfanya awe ametumia jumla ya Pauni 385.5 milioni kwenye usajili wa mabeki wote tangu alipotua kuchukua mikoba ya kuinoa miamba hiyo ya Etihad kwenye Ligi Kuu England.

Kwa mkwanja wote huo aliotumia Guardiola kwenye usajili wa mabeki, utashangaa timu yake ilijitoa kwenye mbio za kumsajili Virgil van Dijk kisa tu waliambiwa walipe Pauni 75 milioni, kitu ambacho Liverpool ilikifanya na sasa imefanikiwa kuwa na ukuta wa zege huko Anfield ilipomnasa kutoka Southampton.