Pep awapa mizuka Man U kwa Maguire

Muktasari:

City wameripotiwa kuingia kiujanja katika vita ya kumsajili beki huyo kutoka Leicester City kwa kutengeneza ofa ambayo haitaikuza sana bei ya Maguire.

MANCHESTER, ENGLAND.KILA uchao kuna mambo mapya kwenye mbio za usajili na mara hii Manchester United wamepewa fursa ya kutabasamu kidogo baada ya Pep Guardiola kupuuza ripoti kwamba wanataka kumsajili Harry Maguire.
Man United wanaona kizingiti kikubwa katika mbio za kumpata beki tano huyo ni Man City ambao wanasemekana wameweka ofa ya mtego ambayo inawaangalia tu Mashetani Wekundu watakachotoa nao, wanatoa hicho hicho kisha Maguire achague pa kwenda.
City wameripotiwa kuingia kiujanja katika vita ya kumsajili beki huyo kutoka Leicester City kwa kutengeneza ofa ambayo haitaikuza sana bei ya Maguire.
Imeripotiwa kuwa City wanajua wakitangaza ofa yao, itaanza vita ya kupandiana dau kati yao na United, jambo ambalo litamfanya beki huyo Muingereza auzwe ghali sana, hivyo wameamua kuweka dau sawa na la United walioweka ofa ya Pauni 70 milioni, na kisha kumuacha Maguire achague kucheza Ligi ya Mabingwa na City ama Europa Ligi na United.
Lakini akizungumza jana, kocha wa City, Pep amesema: "Tuna furaha na kikosi tulichonacho. Sijui kama kuna wachezaji wapya watakuja. Lakini nina furahia wachezaji tulionao.
"Kuna nafasi (ya beki kuja) lakini sijui kama inawezekana. Tayari tunao mabeki watatu wazuri na Fernandinho anaweza kucheza katika nafasi hiyo pia."