Pep awaambia wazi Spurs hawana chao

Muktasari:

  • Liverpool waliing’oa City katika hatua kama hiyo mwaka jana, lakini bosi huyo wa Etihad amesisitiza hamna jambo kama hilo tena msimu huu.

MANCHESTER,ENGLAND. PEP Guardiola buana anajiamini sana. Kama unamchukulia poa kwenye mambo yake wewe mcheki hapa. Kuelekea mechi ya marudiano ya robo-fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya timu yake ya Manchester City na Tottenham Hotspur, jamaa keshamjua mshindi.

Anakwambia Tottenham kwanza watakula kichapo cha mbwakoko kwenye Uwanja wa Etihad leo usiku, kisha Man City watatinga nusu-fainali kwa kunata.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu England walilala 1-0 ugenini kwenye Uwanja mpya wa Tottenham Jumanne iliyopita, kupitia bao pekee la Son Heung-min dakika ya 79.

City ndiyo waliopewa nafasi ya kusonga mbele, huku wachambuzi wengi wakiitabiria timu hiyo hata kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza katika historia yao msimu huu. Hata hivyo, Spurs walipiga mpira mwingi wakikiendesha puta kikosi cha Pep na sasa City wanakabiliwa na hatari ya kutolewa tena mapema dhidi ya timu ya England wenzao kwa mwaka wa pili mfululizo.

Liverpool waliing’oa City katika hatua kama hiyo mwaka jana, lakini bosi huyo wa Etihad amesisitiza hamna jambo kama hilo tena msimu huu.

City wanafukuzia kutwaa makombe manne msimu huu, baada ya kutetea Carabao Cup mwezi Machi, wakitinga pia fainali ya Kombe la FA na kuingia katika raundi tano za mwisho za Ligi Kuu England huku ubingwa ukiwa mikononi mwao.

Ushindi wa 3-1 ugenini dhidi ya Crystal Palace Jumamosi iliyopita atakuwa ni jibu zuri dhidi ya kipigo walichopata kutoka kwa Spurs wiki iliyopita na wanatarajiwa kucheza kwa kiwango cha juu katika mechi ya marudiano leo. Ijumaa iliyopita Guardiola alikanusha madai ya Ilkay Gundogan City “presha ziko sana” wanapocheza mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini aliafiki mwendo wao katika michuano hiyo ya Ulaya si wa kuridhisha. “Soka ni shule isiyo na mwisho; mara nyingine unafaulu, mara nyingine unafeli,” alisema.

Rekodi baina yao

Kufikia sasa, Man City na Tottenham zimekutana mara 41. City wameshinda mara 15, Tottenham wameshinda mara 20. Mechi 6 zilimalizika kwa sare.

Man City

Guardiola leo atamkosa Claudio Bravo, kwa vile kipa huyo raia wa Chile bado hajawa fiti kucheza, huku pia Fernandinho ataangaliwa hadi dakika ya mwisho.

Kocha huyo wa City anatarajiwa kufanya mabadiliko kadhaa ukilinganisha na kikosi kilichocheza mechi ya awali na kulala London kwa ajili ya mechi yao ya leo ambayo ni lazima washinde.

Oleksandr Zinchenko amerejea baada ya kupona majeraha na huenda akaanza badala ya Fabian Delph katika beki ya kushoto, wakati Bernardo Silva, Kevin De Bruyne na Gabriel Jesus wanatarajiwa kuanza.

Tottenham

Harry Kane alilazimika kutoka katika mechi yao ya kwanza mjini London baada ya kuumia enka na huenda asicheze tena msimu huu, wakati Dele Alli alivunjika mkono, lakini bado anaweza kucheza na kifaa maalumu cha kukinga mkono.

Fernando Llorente alitoka nje katika dakika za lalasalama dhidi ya Huddersfield na atafanyiwa vipimo, lakini Mauricio Pochettino hawezi kuwatumia Eric Dier, Serge Aurier na Erik Lamela.

Son Heung-Min aliingia katika dakika za mwisho dhidi ya Huddersfield na anatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya Spurs, huku Lucas Moura akisukuma mambo kuwania kuanza baada ya kutupia ‘hat-trick’ katika ushindi wa 4-0 wikiendi.

- Tottenham walikuwa sare katika mapumziko katika mechi zao tatu zilizopita za Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini mwisho walishinda zote.

- Tottenham hawajaruhusu goli katika mechi zao tatu zilizopita za Ligi ya Mabingwa.

- Tottenham wameshinda mechi tano kati ya sita zilizopita za Ligi ya Mabingwa Ulaya.

- Man City wamefunga angalau magoli mawili katika mechi saba kati ya nane zilizopita walizocheza nyumbani dhidi ya Tottenham katika michuano yote.