Pesa siyo kila kitu! Pep atumia pauni 800mil kusajili City yakosa ubingwa Ulaya

Muktasari:

  • Guardiola ametumia pesa nyingi kwa misimu sita ya hivi karibuni akijaribu kutengeneza timu yenye uwezo wa kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya

Manchester, England. Kocha Pep Guardiola ameshambuliwa vikali na magazeti ya Hispania wakidai amepoteza bure tu Pauni 800 milioni alizotumia kujaribu kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2011.

Ni miaka minane imekatika tangu mara ya mwisho Guardiola alipobeba ubingwa wa Ulaya alipokuwa na Barcelona ilipowasambaratisha Manchester United kumpa taji lake la pili la Ulaya akiwa kocha huku kwenye kikosi chake kulikuwa na mastaa matata kama Lionel Messi, Andres Iniesta, Xavi na Carles Puyol.

Gazeti ya Hispania yameonyesha kutofurahishwa na namna Guardiola alivyotumia pesa nyingi kwa misimu sita ya hivi karibuni akijaribu kutengeneza timu yenye uwezo wa kubeba ubingwa huo wa Ulaya.

Lakini, usiku wa Jumatano iliyopita timu yake ya Manchester City ilitupwa nje na Tottenham Hotspur, ambayo imevuka madirisha mawili bila ya kufanya usajili wowote chini ya kocha wao Mauricio Pochettino.

Guardiola alianzia huko Bayern Munich kusaka ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na kushindwa hadi sasa akiwa na Man City, ambapo kikosi chake kimeruhusu mabao 27 katika mechi 12 za mtoano ambazo ameishia kutupwa nje tu katika misimu sita ya karibuni.

Wakati anamsajili Riyad Mahrez kwa Pauni 60 milioni zilimfanya kocha huyo awe amefikisha matumizi ya Pauni 800 milioni katika klabu hizo mbili alizozinoa tangu alipoondoka Barcelona.

Wachezaji wengine aliowanasa kwa pesa nyingi ni Aymeric Laporte (Pauni 57 milioni), Bernardo Silva (Pauni 43 milioni), Kyle Walker (Pauni 45 milioni), Benjamin Mendy (Pauni 49.3 milioni na John Stones (Pauni 47.5 milioni).