Pep amsaka beki Maguire nafasi ya Kompany

Muktasari:

  • Ughali wa Maguire unatokana na umri wake wa miaka 26 pamoja na utaifa wake wa England ambapo wachezaji wengi kutoka nchini humo wamekuwa ghali zaidi kwa kile kinachodaiwa kuelewa kwa haraka tamaduni za soka lao.

London, England. Mbabe mmoja anatoka, mbabe mwingine anaingia. Ndicho ambacho kocha wa Manchester City, Pep Guardiola anachotaka kufanya katika dirisha hili la uhamisho. Hatanii na wala hana masikhara, na yuko tayari kutoa pesa nyingi kwa ajili ya jambo hilo.

Baada ya nahodha wake, Vincent Kompany kutangaza kuondoka Etihad baada ya kucheza klabuni hapo kwa miaka 11 yenye mafanikio ikiwemo kutwaa ubingwa wa England kwa mbinde hizi karibuni, Guardiola sasa anahemea saini ya mlinzi nguli wa Leicester City na timu ya taifa ya England, Harry Maguire.

City wapo tayari kutoa dau la pauni 75 milioni kwa mlinzi huyo ambaye dirisha kubwa lililopita alitakiwa kwa nguvu zote na wapinzani wao Manchester United, lakini inajulikana kwamba Leicester wanataka City wavunje rekodi ya uhamisho ya dunia kwa mabeki kwa ajili ya kuinasa saini yake.

Leicester watataka dau la pauni 80 milioni na zaidi kwa ajili ya kumruhusu Maguire kuondoka King Palace na dau hilo litalipiku dau la pauni 75 milioni ambalo Liverpool walitumia Januari mwaka jana kuvunja rekodi ya uhamisho ya dunia kwa walinzi wakati walipomnunua staa wa kimataifa wa Uholanzi, Virgil van Dijik kutoka Southampton.

Ughali wa Maguire unatokana na umri wake wa miaka 26 pamoja na utaifa wake wa England ambapo wachezaji wengi kutoka nchini humo wamekuwa ghali zaidi kwa kile kinachodaiwa kuelewa kwa haraka tamaduni za soka lao.

Maguire amekuwa chaguo la kwanza la Guardiola kuchukua nafasi ya Kompany na kocha huyo alidirikia hata kumfuata uwanjani staa huyo katika pambano dhidi ya Leicester hivi karibuni akimueleza alivyokoshwa na kiwango chake.

Huu ni mwendelezo wa Maguire kung’ara baada ya kutamba katika michuano ya kombe la dunia na kikosi cha timu ya taifa ya England katika michuano ya kombe la dunia nchini Russia katikati mwaka jana ambapo United walianza kumfukuzia kwa kasi.

Hata hivyo Maguire alisaini mkataba mpya wa miaka mitano na Leicester Septemba mwaka jana baada ya uhamisho wake wa kwenda Old Trafford kushindikana na mkataba huo umeiweka Leicester katika nafasi nzuri ya kutomuuza kwa bei rahisi.

Leicester waliweka ngumu wakati City walipomtaka winga wao wa kimataifa wa Algeria, Riyad Mahrez katika dirisha dogo la Januari ambapo walizitia kapuni ofa zao mbalimbali kabla ya kuamua kumuuza katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka jana ambapo waliikamua City pauni 60 milioni ambazo mpaka sasa ni rekodi ya uhamisho klabuni hapo.

Kocha wa Leicester City, Brendan Rodgers ni shabiki mkubwa wa  Maguire, 26, na Leicester wana historia ya kuwatilia ngumu wachezaji wao pindi wanapotakiwa na klabu mbalimbali nyingine ikiwemo Manchester City yenyewe.

Rodgers amedai kwamba anajua kuwa wachezaji wake, hasa Maguire watatakiwa na klabu mbalimbali kubwa lakini akadai kwamba atalishughulikia jambo hilo kwa ukweli mkubwa.

“Unachoweza kufanya kwa sasa ni kuangalia uwezekano wa sasa hivi. Nimewahi kuwa katika hali kama hii zamani ambapo wachezaji wako wanahusishwa kwenda timu kubwa na unajaribu kuwa mkweli katika hali hiyo.” Alisema Rodgers ambaye ni kocha wa zamani wa Liverpool.

“Nitaongea na mchezaji kama ninavyoongea na mwanangu wa kiume. Nitawaambia kuhusu uwezekano wa wao kubaki na jinsi hali inavyoweza kuwa wakiondoka. Wao ni wanaume kwahiyo wataamua wao wenyewe.” Alisema Rodgers.