Pep amchezea akili Klopp

Tuesday February 12 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND.KOCHA, Pep Guardiola amesema tena kwa msisitizo kwamba, Liverpool ya Jurgen Klopp bado wana nafasi kubwa ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Guardiola amesema hilo baada ya kushuhudia kikosi chake cha Manchester City kikiikandamiza Chelsea 6-0 kwenye mchezo wa ligi hiyo juzi Jumapili na kurudi kileleni kwa msimamo wa ligi kwa kishindo.

Katika mechi hiyo, straika Sergio Aguero alipiga hat-trick, Raheem Sterling alitupia mbili na moja aliweka kambani Ilkay Gundogan huku Chelsea ikitoka patupu na kuwafanya kukumbana na kipigo kizito zaidi katika historia yao ya Ligi Kuu England.

Hata hivyo, Guardiola bado haamini kama Man City watachukua ubingwa na kusema Liverpool ndiyo watakaobeba, akisema: “Tumecheza mechi moja zaidi na Liverpool wao ndio wenye nafasi kubwa ya kuendelea kufukuzia taji.

“Kama watashinda mechi zao zote, watakuwa mabingwa. Kitu ambacho tunapaswa kufanya ni kushinda mechi zetu. Hivyo nadhani mwisho wa msimu mambo yatakuwa magumu na hapo itajulikana itakavyokuwa kuhusu ubingwa.

“Kuwa kileleni ni kitu muhimu. Baada ya ile mechi dhidi ya Newcastle, kila mtu alisema zitakuwa pointi saba, huku sisi tulikuwa na mechi dhidi ya Arsenal na Chelsea zinafuatia na zilikuwa mechi ngumu sana. Lakini, baada ya Liverpool kushindwa kuwafunga Leicester City jambo hilo limetupa nafasi na nguvu mpya ya kutaka ubingwa.”

Advertisement