Penzi la Nandy na Ruge limezima ghafla

Muktasari:

  • Msanii huyu ameeleza kuwa awali alipata wakati mgumu kumkubali Ruge kutokana na aliyokuwa akiyasikia kumhusu lakini taratibu akamuelewa na kumuona kuwa ni mtu sahihi.

Hakika Nandy alikolea kwa Ruge, hivi ndivyo tunavyoweza kusema maana kwa hadithi hii tamu ya mapenzi hakuna maneno mengine yanaweza kutumika.

Nandy amepiga stori na Millard Ayo na kueleza kwa kina kuhusu uhusiano huo uliodumu kwa muda wa miaka mitatu na ukakoma mwezi mmoja kabla ya kurasimishwa rasmi na ndoa.

Msanii huyu ameeleza kuwa awali alipata wakati mgumu kumkubali Ruge kutokana na aliyokuwa akiyasikia kumhusu lakini taratibu akamuelewa na kumuona kuwa ni mtu sahihi.

“Alikuwa ananitumia meseji nikawa nafanya kama sizioni, ikapita muda kuna siku akaamua kuniita sehemu ili tuzungumze uso kwa uso nikamsikiliza na huo ndiyo ukawa mwanzo wa ukaribu wetu kama wapenzi,”

Licha ya kuwa walikuwa wakipendana sana kuna wakati walipishana lakini ugomvi wao haukuwahi kudumu kwa zaidi ya saa tatu bila kupatana.

“Ilikuwa inatokea tunapishana ila hatujawahi kuwa kwenye ugomvi kwa zaidi ya saa tatu bila kupana na chanzo kikubwa cha ugomvi inakuwa kutopokea simu na mara nyingi tatizo hilo linakuwa kwangu,”

Nandy amekwenda mbele zaidi na kueleza kuwa uhusiano wake na Ruge ulikuwa bora kuliko mahusiano mengine yote aliyowahi kupita pengo la mwanaume ni kubwa mno kwake.

Amesema, “Namkumbuka kwa mengi alikuwa ni mtu anayejua na kufuatili vitu vingi, yani hata mawazo yangu mtu wa kwanza kumwambia ni yeye hata kama ni pumba ananisikiliza hadi mwisho halafu ananishauri, nikiwa na huzuni namfuata yeye hata umbea namwambia lakini sasa hivi kuna wakati nakutana na vitu natamani nimwambie ila ndio nashindwa,”

Amesema Ruge alikuwa akivutiwa na namna binti huyo anavyomtanguliza Mungu mbele katika maisha yake na wakati mwingine alikuwa akimkumbusha kwenda kanisani.

“Yani hata kama yeye haendi kanisani alikuwa anafurahi kuniona mimi nikienda na wakati mwingine hata kunikumbusha, kuna muda nilikuwa nasali nae pamoja, namuombea hata kumletea maji ya baraka yaliyoombewa,”

Pia uchapakazi wangu ulikuwa ukimvutia sana nadhani hivyo vitu ndivyo vilimfanya anipende wakati mimi kwake nilipenda jinsi alivyoweza kuongoza maisha yangu, kunisimamia nitimize ndoto zangu na alikuwa mkweli mno,

“Amesema Ruge alikuwa mtu anayekiri kama amefanya kosa , suala hili lilikuwa likinipa moyo na pia alikuwa akiwapenda sana watoto wake na pia nilikuwa nakutana nao,”