Pengo la Kane litazibwa na hawa England

Muktasari:

Tayari Kocha wa Tottenham Spurs, Jose Mourinho ameshaweka wazi klabu yake haina uhakika wa muda rasmi ambao Kane atarudi uwanjani baada ya kufanyiwa upasuaji.

LONDON, ENGLAND . UKISIKIA majanga ndiyo haya wanayokutana nayo England, maana kuna kila dalili ya kwenda Euro 2020 bila nahodha na straika wake tegemeo, Harry Kane.

Ndiyo, majeraha ya nyama za paja aliyoyapata juzi kati akiwa na Tottenham Hotspur katika mchezo dhidi ya Southampton yanahatarisha nafasi yake ya kuiongoza England katika michuano ya Euro 2020.

Tayari Kocha wa Tottenham Spurs, Jose Mourinho ameshaweka wazi klabu yake haina uhakika wa muda rasmi ambao Kane atarudi uwanjani baada ya kufanyiwa upasuaji.

Mourinho anadai Kane anaweza kurudi Aprili, Mei, Juni au hata msimu ujao inategemea na jinsi mwili wake utaendana na tiba aliyopewa hadi sasa, lakini kwa ujumla haijulikani lini atarudi uwanjani.

Wakati afya ya Kane ikiendelea kuwa tatizo Kocha wa England, Gareth Southgate anatakiwa kuanza kujiandaa kwenda kwenye michuano hiyo bila straika na kiongozi wa kikosi chake.

Kane amekuwa na mchango mkubwa sana katika mbio za England kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya Euro 2020, maana mbali na kuwa nahodha pia ndiye alikuwa mfungaji wao tegemeo akifunga mabao 12 katika mechi za kufuzu.

Lakini ndiyo hivyo tena Kane ni majeruhi na lazima, Southgate apate mchezaji wa kuziba nafasi ya Kane na kuongoza mashambulizi ya England timu yake katika michuano hiyo.

Hadi sasa, majina matano ndiyo yanatajwa zaidi kuziba pengo la Kane ikiwa atashindwa kupona kwa kabla ya kuanza kwa michuano ya Euro 2020.

Marcus Rashford

Marcus Rashford alisheherekea kucheza mechi yake ya 200 akiwa na kikosi cha Manchester United kwa kufunga mara mbili wakati timu yake ikishinda kwa mabao 4-0 dhidi ya Norwich katika mchezo wa Ligi Kuu England.

Akiwa na umri wa miaka 22 tu, Rashford amekuwa mchezaji tegemeo katika kikosi cha Ole Gunnar Solskjaer huku akitabiriwa kufanya makubwa zaidi siku za usoni.

Tayari Rashford amefunga mabao 10 katika kikosi cha Timu ya Taifa ya England katika mechi 38 alizocheza hadi sasa na kikubwa kinachotakiwa kwake ni kukomaa tu kabla ya kupewa majukumu ya kuongoza taifa lake.

Kama Kane akiwa hajawafiti au akikosekana kabisa basi Southgate anaweza kumtumia Rashford kama straika wa kati na kumtoa pembeni ambako amekuwa akimtumia katika miaka ya karibuni.

Raheem Sterling

Hadi sasa straika huyu wa Manchester City ameshacheza mechi zaidi ya 50 akiwa na kikosi cha England na kufunga mabao 12.

Staa huyo mwenye umri wa miaka 25, anaendelea kuwa roho ya safu ya ushambuliaji ya Man City na mchezaji muhimu katika mipango ya ushambuliaji ya Southgate.

Tatizo, pekee ni kuwa Sterling amekuwa akitumika zaidi pembeni, lakini kama ilivyo kwa Rashford, anaweza kuandaa mfumo sahihi ambao utamfanya Sterling akatisha akicheza kama straika wa kati.

Lakini, ili hilo lifanikiwe ni lazima Southgate, aje na mfumo unaotegemea zaidi pasi na mashambulizi ya kushtukiza huku nafasi za magoli zikitengenezwa kutokea katikati ya uwanja na kuepuka kutumia krosi kwa sababu ya kimo Sterling.

Tammy Abraham

Straika huyo wa Chelsea anaweza kuwa ndiyo kwanza amecheza mechi nne tu za timu ya taifa lakini Abraham anaonekana kuwa na kipaji kikubwa sana.

Hadi sasa tayari amefunga mabao 13 kwenye Ligi Kuu England akiwa kwenye kikosi cha Chelsea na kama akiendelea kuaminiwa atakuwa mshambuliaji tishio sana.

Kocha wa Chelsea, Frank Lampard anaamini Abraham ana uwezo mkubwa wa kucheza kama mshambuliaji wa kati na kusimama peke yake, kama Southgate akiamua kumuamini huyu ni aina ya straika ambaye kwa kiasi fulani anafanana na Kane kiuchezaji.

Danny Ings

Japokuwa straika wa Bournemouth, Callum Wilson amekuwa akiitwa mara kwa mara England kuwa kama mbadala wa Kane, lakini kwa sasa kelele za kutaka Ings ajumuishwe kwenye kikosi cha Euro 2020 zinazidi kushika kasi.

Straika huyo wa zamani wa Burnley na Liverpool tayari ana mabao 14 kwenye Ligi Kuu England msimu huu akiwa na kikosi cha Southampton.

Licha ya kuwa na miaka 27, Ings amewahi kucheza England mara moja tu, hii ilikuwa mwaka 2015 katika mchezo dhidi ya Lithuania. Mechi za kirafiki za kujiandaa na Euro 2020, dhidi ya Italia na Denmark, Machi mwaka huu zinaweza kumpa nafasi Southgate kupima kama Ings atafiti kwenye mfumo wake.

Jamie Vardy

Straika huyu wa Leicester City amekuwa kwenye kiwango bora sana msimu huu, Vardy amefunga mabao 17 hadi sasa msimu huu akiwa na kikosi cha Kocha Brendan Rodgers.

Tatizo pekee kwa Vardy ni kuwa baada ya Kombe la Dunia 2018, alitangaza kustaafu kucheza timu ya Taifa England, lakini Southgate anaweza kuamua kumfuata na kumuomba arudi kuchezea timu ya taifa kwenye Euro 2020.

Akiwa na umri wa miaka 33, Vardy bado ana uwezo wa kuibeba England, lakini ni suala la Southgate kumfutana na kufanya naye mazungumzo ya kina ili arudi kuongoza mashambulizi ya England. Vardy anaweza kuwa mtu sahihi.