Pazia la KPL kufungwa kesho, timu tano zakaria kuti kavu

Saturday October 6 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi, Kenya. Tayari Gor Mahia wameshakabidhiwa Uchampioni wa Ligi Kuu Kenya (KPL), msimu wa 2017/18, huku Bandari wao wakijihakikishia nafasi, vita kubwa iliyosalia kwa sasa ni kubaini nani atashuka daraja na nani atasalimika.

Ugumu wa vita hiyo mpaka sasa kuna timu tano ambazo hazina uhakika wa kusalia kwenye KPL msimu ujao na kibaya zaidi ni kwamba, timu mbili kati yao zinakutana uso kwa uso katika mechi ya lala salama.

Miamba hiyo inayokabana koo, kukwepa kuungana na Thika United na Wazito FC ambazo tayari zimeshashuwa daraja, ni Vihiga United, Nakumatt FC, Posta Rangers, Nzoia Sugar na wakata miwa wa Chemelil Sugar.

Timu zote hizo ziko katika hatari ya kumaliza katika nafasi ya 16, na kama hilo likitokea basi itabidi zicheze mechi ya mtoano (Play-off), kupata kibonde. Kwa sasa nafasi ya 16 inashikiliwa na Posta Rangers. Rangers inakutana na Kakamega Homeboyz. Mechi ya kwanza Rangers ilishinda 2-0

Nakumatt itakutana na Vihiga United huku zote zikichungulia mlango wa kutokea kwani tofauti kati yao ni alama moja tu. Mechi ya kwanza, walitoka sare ya 0-0. Atakayepigwa atashuka hadi nafasi ya 16 katika msimamo wa ligi wenye timu 18.

Kwa upande wao, Chemelil Sugar wanabebwa na fomu nzuri ambayo wamekuwa nayo katika siku za hivi karibuni lakini wana kibarua kigumu watakapo wafuata Kariobangi Sharks. Ikumbukwe kuwa katika mechi ya raundi ya kwanza, Sharks walilazimisha sare ya 1-1, ugani Chemelil Sugar Complex.

Wakati Chemelil Sugar wakiwa na kibarua kigumu dhidi ya Sharks, wakata miwa wenzao Nzoia Sugar walibahatisha sare ya 2-2 dhidi ya AFC Leopards, katika mchezo wa raundi ya kwanza ya ligi, wanaingia ugani kesho kuumana na Ingwe huku wakiwa hawana huduma ya mfungaji wao hatari, Elvis Rupia, aliyetimkia nchini Zambia.

Itakumbukwa kuwa katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, mabao ya Nzoia yalitiwa kimiani na Rupia, kabla Ingwe hawajazinduka na kusawazisha kupitia kwa Brian Marita na Robinson Kamura.

Advertisement