Pazi amtaka Chama katika ubora wake kwa AS Vita

Muktasari:

Chama amekuwa katika kiwango cha kawaida katika mechi za hivi karibuni kiasi cha mashabiki kushangazwa na hali hiyo huku wengine wakijiuliza nini kimempata mchezaji huyo maarufu kama Mwamba wa Lusaka.

Dar es Salaam. Kipa wa zamani wa Simba, Idd Pazi amesema kocha Patrick Aussems anatakiwa kumrejesha kiungo Clatous Chama katika nafasi yake eneo la katikati ili arejee katika ubora wake.

Chama amekuwa katika kiwango cha kawaida katika mechi za hivi karibuni kiasi cha mashabiki kushangazwa na hali hiyo huku wengine wakijiuliza nini kimempata mchezaji huyo maarufu kama Mwamba wa Lusaka.

Tangu Chama alipofunga bao katika mchezo wa kufuzu hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nkana Devils ya Zambia hajafanya hivyo tena huku kiwango chake kikiporomoka katika michezo mitatu iliyopita ya hatua ya makundi.

Katika mchezo huo uliofanyika Dar es Salaam, Simba ilishinda mabao 3-1 na kufuzu hatua ya makundi huku Chama akifunga bao moja na kuhusika katika mabao mengine mawili yaliyofungwa na Jonas Mkude na Meddie Kagere.

Awali mchezaji huyo alikuwa akicheza kama kiungo mchezeshaji kutokea katikati ya uwanja wakati kwa siku za karibuni Aussems amekuwa akimchezesha kama winga wakati mwingine wa kushoto au kulia kulingana na mchezo husika.

Pazi alisema kiwango cha Chama si kama kile ambacho watu wamekizoea hivyo kumshauri kocha Aussems kumrejesha katika nafasi yake ili kurejesha ubora wa mchezaji huyo.

"Sasa hivi Chama anavyocheza sio yule ambaye wengi tulizoea kumuona akicheza kwa kiwango kikubwa nafikiri ni kutokana na kubadilishwa nafasi sasa kocha anatakiwa kumrejesha katika nafasi yake ya awali ili arejee katika ubora wake," alisema Pazi.