Pata,kosa ya usajili wa ED Woodward huko Old Trafford

Muktasari:

  • Lakini kama ungekuwa mwalimu wa Woodward kwa kutazama usajili wa wachezaji wake aliowasajili Man United, wapi ungewaka PATA na wapi KOSA. Cheki mastaa wake wote aliowasajili.

MANCHESTER,ENGLAND.ED Woodward yupo kwenye presha kubwa huko Manchester United ambapo mabosi wake wamekuwa wakimtazama kwa karibu kama anafaa kuendelea kufanya kazi kwenye timu hiyo au afutwe.

Makamu mwenyekiti huyo wa Man United anafuatiliwa kwa karibu na wamiliki wa timu, familia ya Glazers hasa katika kipindi hiki cha usajili wa wachezaji baada ya kuonekana wachezaji wake anaowasajili wamekuwa wakiingizia tu timu hasara.

Woodward usajili wake wote wa pesa nyingi umekuwa na makosa kwa kuanzia kwa Fred, Paul Pogba, Angel Di Maria hadi kwa Romelu Lukaku. Mastaa hao wameigharimu Man United pesa nyingi sana, lakini kwa huduma zao za ndani ya uwanja ni majanga makubwa.

Lakini kama ungekuwa mwalimu wa Woodward kwa kutazama usajili wa wachezaji wake aliowasajili Man United, wapi ungewaka PATA na wapi KOSA. Cheki mastaa wake wote aliowasajili.

Marouane Fellaini, Pauni 27.5 milioni

Licha ya kuwa Old Trafford kwa miaka sita na kucheza zaidi ya mechi 100 za Ligi Kuu England, Fellaini ameshindwa kuingia kwenye orodha ya wachezaji muhimu zaidi katika kikosi cha Man United. Alisaidia timu hiyo kubeba Europa League mwaka 2016-17 na Kombe la FA 2015-16, lakini zaidi ya hapo kiwango chake Big Fela kilikuwa shida. KOSA.

Juan Mata, Pauni 37.1 milioni

Alisajiliwa kutoka Chelsea mwaka 2014 ikiwa ni moja ya usajili muhimu kabisa uliofanywa na Man United katika kipindi timu ilipokuwa chini ya David Moyes. Mata anaondoka Man United akiwa mmoja kati ya wachezaji waliojitahidi kucheza kwa kiwango cha juu kwa muda wote waliokuwa kwenye timu hiyo licha ya majanga. PATA.

Ander Herrera, Pauni 28.8 milioni

Kama ilivyo kwa Juan Mata tu. Man United imepata wachezaji wazuri katika nyakati za hovyo kabisa baada ya kufanikiwa kuwa na huduma ya staa wa Kihispaniola, Ander Herrera. Kiwango cha mchezaji huyo kimekuwa hakina mashaka licha ya kwamba amekuwa akiingia na kutoka katika kikosi cha wababe hao wa Old Trafford. Anaondoka. PATA.

Luke Shaw, Pauni 33 milioni

Alikumbwa na majeruhi pamoja na kukosolewa kuhusu utimamu wake wa mchezo siku zake za mwanzoni kwenye kikosi hicho cha Old Trafford. Lakini, baadaye, Luke Shaw aligeuka na kucheza mpira mkubwa unaomfanya asiwemo kwenye ile orodha ya wachezaji wanaoweza kufunguliwa mlango wa kutokea kwenye timu.

PATA.

Marcos Rojo, Pauni 16 milioni

Majeruhi, kushindwa kuwa kwenye kiwango bora ni mambo kadhaa yaliyomtibulia Muargentina, Rojo kupata nafasi huko kwenye kikosi cha Man United. Pengine Rojo amekuwa hana bahati na timu hiyo ya Old Trafford licha ya kuonyesha kiwango kizuri mara chache alizocheza. Kwa sasa yupo kwenye orodha ya wachezaji wanaoondoka.

KOSA.

Angel Di Maria, Pauni 59.7 milioni

Di Maria alivunja rekodi ya uhamisho England wakati aliposajiliwa kwa Pauni 60 milioni akitokea Real Madrid mwaka 2014. Hata hivyo, Muargentina huyo baada ya kutua Old Trafford amekuwa tofauti kabisa na mchezaji yule aliyekuwa Bernabeu au huyu wa sasa huko PSG. Di Maria alionekana mzigo na alihama baada msimu mmoja tu. KOSA.

Daley Blind, Pauni 14 milioni

Kiraka huyo wa Kidachi alikuwa mchezaji muhimu wakati wake alipokuwa kwenye kikosi cha Man United kabla ya kuuzwa kwenda Ajax. Blind alikuwa na uwezo wa kucheza beki wa kushoto, beki wa kati na pengine kiungo wa kati. Alikuwa akiipa Man United machaguo mengi ndani ya uwanja, lakini akapigwa bei akaondoka. PATA.

Memphis Depay, Pauni 25 milioni

Kipaji maridhawa kabisa, lakini Mdachi huyo alishindwa kuzoea mazingira ya England na alikuwa kichekesho tu huko Man United. Kwa sasa anacheza soka lake tamu kwenye kikosi cha Lyon huko Ufaransa, lakini hilo halikuwezekana alipokuwa Old Trafford na hakuweza kudumu sana akaondoka haraka sana kutimkia Ufaransa. KOSA.

Matteo Darmian,Pauni 12.9 milioni

Alisajiliwa kuongeza nguvu kwenye beki ya pembeni ambapo ilikuwa shida kiasi cha kufanya mawinga Ashley Young na Antonio Valencia kubadilishwa na kucheza beki za pembeni. Lakini, Darmian hatakuwa na maisha yenye kumbukumbu tamu kwa muda wake aliokaa huko Old Trafford na sasa anapiga hesabu za kuhama tu. KOSA.

Bastian Schweinsteiger, Pauni 15 milioni

Gwiji huko kwenye soka la Ujerumani na Man United aliponaswa kulikuwa na matarajio mazuri kutoka kwake. Pauni 15 milioni zililipwa huko Bayern Munich ili kupatikana kwa huduma ya kiungo huyo wa soka. Lakini baada ya kutua tu Old Trafford, Schweinsteiger hakuwa na maisha mepesi na kujikuta akiishia kucheza mechi 18 tu katika ligi. KOSA.

Morgan Schneiderlin, Pauni 24 milioni

Alipaswa kuwa mtu muhimu wa kuziba pengo lililokuwa kwenye sehemu ya kiungo ya Man United. Lakini kiungo huyo wa zamani wa Southampton maisha yake ya huko Old Trafford hayakuwa mepesi na kuachana na timu hiyo miaka miwili tu baada ya kusajiliwa, huku akiwa amecheza mechi 32 kwenye Ligi Kuu na kutimkia Everton. KOSA.

Anthony Martial,Pauni 44.5 milioni

Haikuwa kazi nyepesi kwa staa huyo wa zamani wa Monaco, lakini Martial amejitahidi kucheza kwa kuzingatia kiwango cha pesa kilicholipwa kupata saini yake. Hakika Man United ililipa pesa nyingi, hivyo Martial alipambana asiwe mchezaji wa hovyo aliyesajiliwa kwa pesa ndefu kwa ile huduma yake huko Old Trafford. PATA.

Eric Bailly, Pauni 30 milioni

Kama isingekuwa majeraha, Bailly angekuwa bonge la beki wa kati katika kikosi hicho cha Man United na kwenye Ligi Kuu England. Lakini, sasa majeruhi yamemtibulia. Hata hivyo, mara zote ambazo Bailly amecheza, Man United ilikuwa kwenye mikono salama kitu ambacho mashabiki wake wanaomba muda wote beki wao awe fiti. PATA.

Ibrahimovic, bure

Huna kingine zaidi ya kusema Zlatan alifanikiwa kurudisha furaha kidogo huko Old Trafford baada ya kufunga mabao 17 katika mechi 33 alizocheza kwenye Ligi Kuu England. Aliisaidia timu timu hiyo kushinda Kombe la Ligi na Europa League na kuwafanya mashabiki kuwa na furaha. Hata hivyo, Zlatan akakatisha furaha yao. PATA.

Henrikh Mkhitaryan, Pauni 30 milioni

Alinaswa kutoka Borussia Dortmund na hakika saini yake iliwafanya mashabiki wa Man United kushangilia sana kutokana na rekodi zake huko kwenye Bundesliga. Lakini, alipotua tu Old Trafford amekuwa mchezaji wa kawaida sana kiasi cha kuwafanya Man United hata kushawishika kumbadilishana na Arsenal kumchukua staa Sanchez. KOSA.

Paul Pogba, Pauni 89 milioni

Rekodi ya dunia ya uhamisho ilivunjwa wakati Man United inafanikiwa kunasa huduma ya Paul Pogba kutoka Juventus mwaka 2016. Zililipwa Pauni 89 milioni. Kwenye kikosi hicho cha Man United, kiwango cha Pogba kimekuwa kama homa za vipindi, kinapanda na kushuka huku akidaiwa kuwa chanzo cha migogoro. KOSA.

Victor Lindelof,Pauni 31 milioni

Man United bayana kabisa imeonekana kuwa na tatizo kubwa kwenye safu yake ya mabeki wa kati hata baada ya kumsajili Lindelof kutoka Benfica kwa ada ya Pauni 31 milioni. Mwanzoni ilionekana kama shida hiyo ingekwisha, lakini hakukuwa na afadhali na Man United imekuwa ikiruhusu mabao ya kizembe msimu uliomalizika. KOSA.

Romelu Lukaku,Pauni 75 milioni

Baada ya kuongoza vyema fowadi ya Everton, Man United ilishawishika na kulipa Pauni 75 milioni kupata saini yake. Mashabiki wa Man United walifurahi sana kupata huduma yake, lakini baada ya kutua Old Trafford, Lukaku amekuwa hana maajabu. Kuna wakati amejikuta hata akiwekwa nje ya kikosi mbele ya Marcus Rashford. KOSA.

Matic, Pauni 40 milioni

Akiwa mtulivu mpira unapokuwa kwenye miguu yake, huku akifanya kazi muhimu zaidi ya kuwalinda mabeki, staa huyo wa Kiserbia amekuwa mmoja wa watoa huduma bora kwenye kikosi hicho cha huko Old Trafford. PATA.

Sanchez, kubadilishana

Sanchez anaigharimu Man United Pauni 505,000 kila wiki kutokana na mkataba wake aliosaini kwenye kikosi hicho baada ya kujiunga na kwa dili la kubadilishana wachezaji ambapo Arsenal wao huko alikotoka walimchukua Henrikh Mkhitaryan. Sanchez amefunga bo moja tu kwenye Ligi Kuu England msimu huu na kuwa kimeo. KOSA.

Dalot, Pauni 19 milioni

Hakika Man United ilifanya uamuzi wa busara kwa kumsajili Dalot kwasababu mchezaji huyo atakuwa Old Trafford kwa muda mrefu kutokana na umri. Kiwango chake alichokionyesha kwenye mechi chache alizocheza na pesa aliyonunulia, Dalot amekuwa usajili mzuri kabisa. PATA.

Fred, Pauni 52 milioni

Fred anawachanganya mashabiki wa Man United kwa sababu wakati alipokuwa anasajiliwa walimfurahia sana tofauti na alivyoanza kuichezea timu hiyo. Kiwango cha Mbrazili huyo kimekuwa na mashaka kuonekana kama vile Man United imepigwa tu pesa wakati ilipoilipa Shakhtar Donetsk, Pauni 52 milioni kumsajili. KOSA.

Lee Grant, Pauni 1.5 milioni

Usajili wa kushtukiza kutoka Stoke City mwaka jana. Hakuna aliyekuwa akiamini kama Man United ingefanya usajili wa kipa huyo mkongwe. Amecheza mechi moja tu kwenye kikosi hicho, Kombe la Ligi, wakati Man United ilipochapwa kwa penalti 8-7 dhidi ya Derby. Hakuna alichosaidia kwenye timu hiyo zaidi ya huko mazoezini tu. KOSA.