Papy Tshishimbi: Hiyo Yanga SC mpya watu wataomba poo

SIYO jambo la kawaida kwa wachezaji kukaa muda mrefu hivi bila ya kukutana. Mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19 uliosimamisha mambo mengi umetupa somo kubwa.

Kilichonifurahisha ni hatua ya kila mmoja wetu kupimwa afya yake.

Hakuna namna, ni lazima tumshukuru Mungu kila mmoja na imani yake kwani mpaka mambo yanarejea hakuna taarifa mbaya yoyote kutoka sio timu yangu bali kwa klabu zote nchini. Hii tunapaswa kushukuru. Najua bado kuna wenzetu baadhi hawajawasili lakini habari nzuri ni kwamba tunasikia wako salama huko waliko na tuna imani pia wataungana na sisi wakiwa salama.

Haikuwa hali nzuri kwakweli tangu mlipuko wa virusi hivi vya corona. Taharuki ilikuwa kubwa kwa kila mmoja. Unapoona hali inafikia hata watu kuogopana na kukwepa kuonana, unagundua kwamba wakati tuliopitia haukuwa mzuri kabisa katika maisha yetu. Na huko kwingine bado mambo ni magumu.

Ngoja niwape ushuhuda mmoja. Juzi na jana wakati tunakutana kitu kilichonivutia ni kuona kila mchezaji ana hamu ya kucheza mpira. Kila mtu anatamani ligi ianze sasa. Watu wengi wanaona ile tarehe ya kuanza ligi ipo mbali. Hii inanipa picha kwamba kuna uwezekano hali ya ushindani itakuwa kubwa sana. Acha tuone itakuwaje mpira unachezwa hadharani.

Narudi katika jambo ambalo nilitaka kulizungumzia leo, nitaegemea sana katika klabu yangu ya Yanga ingawa hiki nitakachokizungumzia kinafikisha elimu kwa klabu zote na hata wasimamizi wa mashindano ya Ligi za hapa.

Kuna hawa jamaa wanaitwa GSM tuko nao hapa Yanga kama wadhamini wetu. Nimekuwa nikiwaangalia kwa jicho la kipekee sana kwa mambo ambayo wanayafanya hapa Yanga.

Ukiangalia kama wadhamini wameamua kufanya mambo mengi ambayo tunaambiwa ni nje ya mkataba wao ambao wameingia na Yanga.

Kuna hatua nzuri na kubwa sana ambayo naiona kwao. Hebu angalia kwa nafasi yao kama wadhamini, wanakuja moja kwa moja wakishirikiana na viongozi wa klabu na kusikiliza shida za wachezaji mmoja mmoja na hata kama timu.

Kwasasa nimesikia na kuona kwenye magazeti kwamba ndio wanaosimamia pia usajili, hatua ambayo binafsi nimeipitia na sio tu wanaongea na wewe kuhusu mkataba bali wanakupa elimu ya upana wake katika malengo yao ya huko mbele wanataka kuufanya Yanga kuwa klabu gani lakini pia mimi kama mchezaji kipi wanataka kuona ukikifanya.

Maisha yao kama wadhamini wa klabu yanavutia hata mchezaji kuwa nao karibu kutokana na kujiweka kwao karibu kwa timu na kutatua shida mbalimbali sio rahisi kwao kumpuuza mchezaji yeyote.

Kwenye hili nimpongeze sana Hersi Said huyu jamaa kama Yanga itakuja kuwa klabu ya kisasa zaidi basi anapaswa kubaki katika historia ya mabadiliko makubwa ya hii klabu kwa jinsi kwanza alivyofanikiwa kuiunganisha klabu na hawa kampuni yake.

Hatua inayovutia zaidi sasa tumeambiwa Yanga itakuwa klabu ya kisasa katika kubadilisha mfumo wa uendeshaji. Wanatamani kuona Yanga inajiendesha na inasimama vyema kiuchumi.

Hii ndiyo hatua muhimu pengine kuliko zote kwani hapa sasa jina kubwa la klabu kama Yanga litaweza kuendana na hadhi yake kibiashara na jinsi itakavyojiendesha kipekee.

Najaribu kukumbuka maisha ambayo niliyakuta hapa Yanga wakati natua jinsi hali ilivyokuwa kiuchumi. Kiukweli ilikuwa ni hali ngumu sana kwa mchezaji wa kigeni kuiona kama una roho nyepesi ilikuwa ngumu kukubaliana na hali ile.

Kila leo ilikuwa ngumu lakini katika bahati ya kipekee sana Yanga ilibahatika kuwa nao wachezaji wanaojitambua tulipokuwa tunaingia uwanjani tulitambua kwamba hapa ni ofisini kwetu acha tusahau yote na tupambane kwa ajili ya maisha yetu. Kwasasa mambo yamebadilika GSM wametufanya kusahau hayo wamekuwa karibu na timu na kumaliza mambo mengi wakishirikiana na viongozi wetu. Hawa jamaa nadhani sasa ni wakati wa mashabiki wa Yanga na hata wanachama kushikamana nao katika haya ambayo wanataka kuyafanya ndani ya Yanga.

Yanga lazima ibadilishe mfumo wake wa kiuendeshaji hatua hii imechelewa sana lakini hakuna namna wakati wa mabadiliko ni sasa katika kuinusuru hii klabu .

Hatua hii itasaidia mambo mengi sana katika kuhakikisha hata wachezaji watakaokuja kuanzia sasa na huko mbele kutopitia hatua ngumu kama ambavyo ilikuwa huko nyuma.

Akili hii imenifanya kuwa mwepesi hata nilipoitwa kwao kama nahodha mkuu kushauri baadhi ya mambo juu ya wachezaji wapya nikaifanya kwa utulivu mkubwa kwa kigezo kwamba kwasasa wapo watu ambao wanatamani kuona klabu hii inanyooka.

Hili sio la kuachiwa mdhamini mmoja pekee bali wadhamini wengine nao wanatakiwa kuungana nao kwani hata kwao lina msaada mkubwa katika kufanya kazi na klabu ambayo imenyooka na kuendeshwa kwa weledi.

Hakuna kampuni inayoweza kufanya kazi na taasisi ambayo haina utulivu wala haitakuwa na uongozi bora na ule unaoendeshwa kwa usafi.

Bahati mbaya sana hapa Tanzania ndio nimekuja kukuta klabu ina wadhamini wa chache sana. Hii sio kwa klabu tu hata Ligi Kuu nayo inaendeshwa na wadhamini wachache sana na matokeo yake hata upana wa mapato ambayo yangezifanya klabu kupata fedha nyingi nao unakuwa mwembamba. Wadhamini wanatakiwa kushiriki hatua za mabadiliko katika kuzibadilisha klabu.

Hatua ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji haitakiwi kuishia Yanga pekee ni kila klabu inatakiwa kuangalia maisha yake na kubadilika kwa maendeleo ya soka la nchi kwa ujumla hii itasaidia klabu nyingi kuwa nao ushindani bora na sio hizi klabu kubwa mbili pekee.