Panga Chelsea kula vichwa vinne zaidi

LONDON, ENGLAND. CHELSEA ipo kwenye harakati za kuwaacha baadhi ya wachezaji katika dirisha hili baada ya kusajili wachezaji watano, katika harakati za kuboresha kikosi chao ambacho msimu uliopita kilionyesha kiwango kisichoridhisha.

Katika dirisha hili Chelsea imewasajili, Timo Werner, Kai Havertz, Ben Chilwell, Thiago Silva na Edouard Mendy, lakini pia inapambana kuwaondoa wachezaji wengine ili kupunguza gharama za uendeshaji, kwa kuwa wachezaji hao sio chaguo la kwanza la kocha Frank Lampard.

Jumatano iliyopita, Ross Barkley alikuwa ni mchezaji wa kwanza kwenye orodha hiyo kuondoka akijiunga na Aston Villa kwa mkopo wa msimu mmoja.

Wachezaji wengine wanaohusishwa kuwa wanaweza kufuata nyayo zake ni Marcos Alonso ambaye licha ya kuanza vizuri katika misimu yake mitatu ya mwanzo, kwa sasa amekuwa kwenye nyakati ngumu chini ya Lampard.

Mhispaniola huyo ambaye aliisaidia sana Chelsea kuchuku ubingwa chini ya Antonio Conte, maisha yake yanaonekana kuwa kwenye kitendawili kwa kuwa Lampard huwa anapendelea zaidi kumtumia Emerson katika nafasi anayocheza yeye.

Mchezaji mwingine ni Loftus-Cheek ambaye hapo awali alikumbana na majeraha yaliyomfanya asipate nafasi ya kucheza lakini hata baada ya kupona Lampard amethibitisha kwamba Muingereza huyo anahitaji muda mwingi wa kuzoea mazingira huku akiwa anacheza ili kuingia kwenye mifumo yake, jambo ambalo kwake haliwezekani.

“Kuna uwezekano mkubwa akaondoka katika dirisha hili, nadhani hilo ndio litakuwa jambo bora kwake kwa kuwa tunahitaji kufanya vizuri, hivyo sidhani kama nitakuwa namchezesha katika mechi nyingi kama inavyotakiwa acheze kwa sababu ametoka kwenye majeraha,” alisema Lampard.

Lampard pia alizungumza kuhusu beki wake wa kati Antonio Rudiger akisema hajui ni hajui hatima yake klabuni hapo.