Pande mbili za wachezaji wa nje ya nchi

Katika siku za karibuni kumekuwa na mijadala mingi kuhusu mchango wa wachezaji wa nje ya nchi kusaidia kuendeleza soka letu, huku kila mtu akiwa na mtazamo wake.

Miongoni mwa vitu vilivyozua mijadala hiyo ni hali inavyoendelea katika mechi za Ligi Kuu Bara, ambapo hadi sasa tayari ligi hiyo ipo katika mzunguko wa nne.

Kilichoonekana katika mechi hizo nne za mwanzo hasa kwa baadhi ya timu ni mchango huo wa moja kwa moja wa wachezaji wan nje, ambapo kati ya klabu 18 zinazoshiriki ligi hiyo, kuna klabu tatu ambazo hadi mechi za mzunguko wa nne zinamalizika, mabao yote yamefungwa na wachezaji wa kigeni.

Klabu hizo ni Azam FC, Yanga SC pamoja na Namungo FC ambapo hadi sasa zinaenda kucheza mechi za mzunguko wa tano zikiwa na mabao ya kufunga yaliyofungwa na wachezaji wa kigeni tu.

Kwa Azam FC wachezaji waliobeba mzigo huo ni Prince Dube, Ali Niyonzima na Obrey Chirwa huku katika Klabu ya Yanga na Namungo mzigo huo ukibebwa na kina Bigirimana Babikakuhe, Lamine Moro, Michael Sarpong na Mukoko Tonombe.

Hali hiyo imezua mijadala mbalimbali huku baadhi ya mashabiki wa timu hizi wakisifia usajili uliofanyika wa wachezaji hawa ambao umeanza kuonyesha mchango katika mechi za awali.

Hata hivyo wapo baadhi ya mashabiki wa timu nyingine wanaelezea upungufu wa safu za ushambuliaji wa timu pinzani kuwa ndio uliosababisha kutoa nafasi kwa wachezaji hao kufunga magoli, na ndio maana mengine yalifungwa na walinzi kama vile Lamine wa Yanga.

Ieleweke kuwa kila kitu huwa na faida na hasara, hivyo hata jambo hili lililotokea hadi sasa lina faida kubwa katika taswira ya soka la nchi, kwani ni kweli kuwa angalau usajili wa wachezaji wa kigeni umeonekana kuwa na tija kwa klabu.

Siku zote sifa ya mchezaji wa kigeni katika ligi zote duniani ni kuwa na hupaswa kuonyesha uwezo zaidi ya wachezaji wa ndani.

Hivyo kwa wachezaji wa kigeni na hasa katika klabu hizo nilizozitaja inaonyesha taswira kuwa usajili huo ulikuwa ni muhimu, hivyo matukio hayo yanahalalisha usajili wa wachezaji wa nje.

Lakini hata kwa wale wenye mtazamo wa kuwa mabao hayo yamefungwa na wachezaji wa kigeni ni kutokana na uwepo wa upungufu wa washambuliaji wa ndani katika klabu mbalimbali zikiwemo hizo.

Jambo hilo linaonekana kuwa na mantiki kwani bila kuwa na upungufu huo maana yake kuwa wachezaji hao wasingepata nafasi ya kucheza hivyo mapungufu ya wachezaji wa ndani ndio yamefanikisha hilo.

Ukiliangakia jambo hilo kwa taswira zote mbili - kwa maana ya faida na hasara, unaweza kufika mahali ukaona kama vile kuna mazingira ya hamsini kwa hamsini, yaani faida ni asilimia 50 huku hasara ikiwa ni asilimia 50 pia.

Ni kweli kuwa usajili wa wachezaji wengi kutoka nje ya nchi kwa msimu huu umeonekana angalau kukidhi mahitaji ya viwango vya wachezaji wanaotakiwa yaani wenye uwezo zaidi ya wachezaji wa ndani.

Pia upungufu unaozungumzwa ambao kwa miaka ya hivi karibuni umeonekana kuwa na ukweli, kwani tumekuwa tukishuhudia safu za ushambuliaji hasa wa ndani zikibadilika mara kwa mara kutokana na washambuliaji wengi kukosa mwendelezo katika ubora ambao huwa wanauonyesha msimu mmoja.

Hivyo kwa upande wa upungufu kuna hasara nyingine ambayo inaigusa hadi timu ya Taifa na hasa pale tunapotaka kwenda kushiriki fainali Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) na za mataifa ya Afrika zinazohusisha wachezaji wa ndani maarufu kwa jina la Chan.

Madhara hayo husababisha kocha wa timu ya Taifa wakati mwingine kuwa na mabadiliko ya vikosi kila anapoita timu, kwani siku zote kocha wa timu ya Taifa huchagua wachezaji aliothibitisha kuwa ni bora kwa wakati husika kulingana na ratiba ya mechi za timu ya Taifa.

Hivyo madhara hayo yanatakiwa kufanyiwa kazi kuanzia kwa wachezaji wenyewe ambao ndio wahusika wakuu na ubora wa wachezaji wa nje umethibitika kuwana faida lakini pia changamoto kwa wachezaji wa ndani ambao wanatakiwa kuibadilisha changamoto kuwa fursa kwao na kuthibitisha ubora wa kupambana na kuonyesha umuhimu wao katika vilabu vyao na timu ya Taifa.