Pancha kibao, lakini wakipona utawapenda

Muktasari:

Makala hii inaangaziwa wachezaji ambao wamekuwa wakiteswa na majeraha ya mara kwa mara na hata wengine kupungua viwango vyao kutokana na majeraha hayo.

WACHEZAJI wengi huwa wanakutana na tatizo la majeraha na wakati mwingine jambo hilo linasababisha kushuka kwa viwango vyao hasa wanapokaa nje ya uwanja kwa muda mrefu wakiuguza majeraha hayo.

Miongoni mwa majeraha makubwa wanayokutana nayo wachezaji wengi ndani na nje ya Tanzania ni maumivu ya misuli au nyama za paja na maungio ya mguu kwenye sehemu ya kisigino.

Wapo wachezaji wengi kwenye Ligi Kuu Bara ambao wenyewe wanateswa na majanga hayo na muda mwingine wanakaa nje kwa muda mrefu licha ya kuwa wanaporudi moto wao unakuwa ni ule ule.

KMC ni timu ambayo kwa sasa inaongoza kwa kuwa na majeruhi wengi kwenye ligu kuu takribani wachezaji sita wanasumbuliwa na matatizo mbalimbali yanayowafanya kuwa nje ya uwanja mpaka sasa.

Miongoni mwa wachezaji hao ni Charles Ilamfia, Yusuf Ndikumana, mshambuliaji Cliff Buyoya, mlinda mlango Denis Richard na Jean Mugiranenza, wachezaji hao wote ni majeruhi katika kikosi cha KMC.

Hata hivyo wachezaji hao bado wanaendelea kupokea matibabu na wanatarajiwa kurejea hivi karibuni kutokana na wengine kuwa na majeraha ya kawaida ambayo yanawaweka nje kwa muda mfupi.

Makala hii inaangaziwa wachezaji ambao wamekuwa wakiteswa na majeraha ya mara kwa mara na hata wengine kupungua viwango vyao kutokana na majeraha hayo.

Shomary Kapombe

Novemba 18, mwaka jana, akiwa mazoezini, Kapombe aliukanyaga mpira vibaya na kupelekea maumivu ya maungio ya goti, hali hiyo ilisababisha kukosa mchezo dhidi ya Lethoto kufuzu Afcon. Beki huyo wa Simba amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara ila amekuwa na kiwango kile kile anaporejea.

Baada ya kupona Kapombe alijumuishwa kwenye kikosi cha Afcon na kwa bahati mbaya aliumia tena akiwa mazoezi hivyo kukosa michuano yote ya Afcon iliyofanyika nchini Misri.

Kapombe pia alikosa mchezo wa kufuzu Afcon dhidi ya Rwanda mwaka 2017, baada ya kuumia nyonga akiwa mazoezini hivyo kukosa mchezo huo ulioisha kwa sare ya 1-1.

Donald Ngoma

Yanga haikupata huduma sahihi ya mshambuliaji huyu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara ya muda mrefu.Aprili 6, msimu uliopita Yanga ilitangaza kumkosa mshambuliaji huyo kwenye mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Wolaita Dicha kutokana na majeraha.

Septemba 23, 2017 Ngoma aliumia na nafasi nafasi yake kuchukuliwa na Emanuel Martin na alikaa nje kwa takribani mwezi mmoja. Ngoma amekuwa na tatizo la kuumia mara kwa mara ambapo Yanga iliamua kuachana naye na kumtimkia Azam Fc.

Hata baada ya kuijunga na Azam, Ngoma hakuwa fiti kutokana na majeraha ya kisigino ambayo yalimbidi akae nje kabla ya kurejea na kuanza kazi na Azam.

Salim Mbonde

Mbonde alisajiliwa na Simba SC misimu miwili iliyopita akitokea Mtibwa Sugar, chini ya kocha Joseph Omog. Beki huyo kisiki amekuwa na bahati mbaya kwa miaka ya hivi karibuni kutokana na majeraha ya mara kwa mara kibaya zaidi mhuwa anachelewa kurudi Uwanjani anapoumia.

Msimu ulioisha Mbonde hakutumika kutoka na majeraha yanayomsumbua mpaka leo hii hali inayoleta wasiwasi juu ya uwezo wake kuendelea kuwa mzuri kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

Tangu akiwa na Mtibwa Sugar, Mbonde amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya vifundo vya mguu, licha ya kwamba mara nyingine alikuwa akirejea kwa haraka akiwa na timu hiyo wenye maskani yake Morogoro.

John Bocco

Mshambuliaji huyo wa Simba kwa sasa ni majeruhi, amekuwa akisumbuliwa na majeraha ambayo kwa kasi kikubwa hayamuweki nje muda mrefu, tatizo lake kubwa la muda mrefu tangu akiwa Azam Fc ni kifundo cha mguu.

Bocco amekuwa na historia ya kuumia tangu akiitumikia Azam ingawa madaktari wamekuwa wakimtibu kwa haraka hivyo kurejea uwanjani na kuuwasha moto wake wa kupachika mabao.

Licha ya kukutwa na majeraha mara kwa mara Bocco ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu Bara, maumivu yake yamekuwa yakipatiwa tiba kwa haraka hivyo kuendelea kuimarika kila kukicha.

Juma Mahadhi

Pengine kiungo huyo Yanga ndiye anayeongoza kwa kuwa na majeraha ya mara kwa mara ndani ya kikosi hicho na hata baadhi ya mashabiki kumsahau kabisa kutoka na muda mrefu anaokaa nje ya uwanja.

Msimu uliopita kiungo huyo alikaa nje wiki mbili baada ya kuumia katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger na kureja uwanjani. Hata hivyo haikuchukua muda mrefu alipata tena majeraha ambayo mapaka sasa hayajapona.

June 4 mwaka huu, alifikisha siku 139 za majeruhi yake ambayo aliyapata msimu uliopita, hata hivyo tayari ameanza mazoezi mepesi kwa ajili ya kurejea.

Daktari anasemaje

Daktari Mkuu wa klabu ya Azam Fc, Mwanandi Mwankemwa anasema tatizo na Enka linatokana kwa baadhi ya wachezaji kutokuwa na uvungu wa unyayo ( Flat Foots ) hivyo kwao inakuwa rahisi kupata tatizo hilo.

Anasema wapo wachezaji wanaopata Enka kwa kucheza kwenye viwanja vyenye mashimo ambayo hayaonekani kwa urahisi na kuongeza kuwa wakati mwingine ugonjwa huo unatokana na mabadiliko ya mifupa kutokana na umri ambapo tabaka za chokaa hujitegemea kwenye mifupa.

Anaongeza kuwa baadhi ya wachezaji kutovaa vifaa vya kujikinga na Enka kama Enka Sapoti, Bandeji, Plaster inaweza kusababisha pia kuwa na tatizo hilo sugu kwa wachezaji wengi.

Kuna tatizo lingine la wachezaji kushikwa na misuli au nyama za paja kwenye hilo Mwankemwa anasema ni kutokana na mchezaji kuwa na asidi nyingi mwilimi baada ya mtu kufanya sana mazoezi au kushiriki mashindano mengi.

Ushauri wa Mwankemwa

Daktari huyo anashauri wachezaji kunywa maji mengi na kwa wachezaji pamoja na kufanya mazoezi ya mnyumbuliko ( Stretching ) na kupata mapumziko mazuri ya kutosha.

Anashauri makocha wa klabu mbalimbali nchini kuwa na mipangilio mizuri ya mazoezi, kufanya mazoezi mepesi na kupata muda mwingi wa kutuliza mwili baada ya mazoezi makali kwa kila mchezaji.