Pamba yaichakaza AFC ikianza vyema FDL

Muktasari:

Mchezo huo ulikuwa wa kwanza kwa timu hizo, ambapo Pamba wameweza kutumia vyema uwanja wake wa nyumbani.

Mwanza. Bao la Straika Maulid Fadhili alilofunga dakika za nyongeza, zimeifanya Pamba kuanza vyema Ligi Daraja la Kwanza kwa kujihakikishia pointi tatu kufuatia ushindi wa mabao 2-1 walioupata leo Oktoba 10 dhidi ya Arusha FC.

Katika mchezo huo ambao umepigwa dimba la Nyamagana jijini hapa ukiwa wa kwanza katika Ligi hiyo, kila timu ilicheza soka la ushindani na wenyeji kuweza kubaki na ushindi na kuianza vyema harakati zao za kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Pamba ndio walitangulia kupata bao kupitia kwa Sunday Justine dakika ya 12 kisha Arusha FC kusawazisha kupitia kwa John Mbilinyi dakika ya 38 na kufanya mchezo huo kuongeza hali ya ushindani.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa pande zote, ambapo Pamba walionekana kuwa na uchu zaidi ya bao kwa kuwa na presha kubwa, huku Arusha FC wakicheza kwa utulivu haswa kuzuia hatari nyingi zilizolenga lango lao.

Kipa wa Arusha FC, Muntaga Yusuph alijikuta akidondosha chozi kufuatia kufungwa bao la pili ambapo alishindwa kumudu shuti lilopigwa na Fadhili na kupoteza matumaini ya japo pointi moja ugenini.