Pamba yagawa dozi nzito kwa Mashujaa FC

Muktasari:

Ushindi huo wa leo kwa Pamba unaiweka katika nafasi nzuri katika vita ya kuwania nafasi ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao kutoka Kundi B.

Mwanza. Pamba FC imeifanyia kitu mbaya Mashujaa FC kwa kuinyuka mabao 3-1 katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza uliopigwa leo, Jumamosi kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

Mchezo huo uliokuwa mkali Mashujaa walitangulia kupata bao dakika ya 40 kupitia kwa Shaban Yassin kabla ya Geofrey Julius kuisawazishia Pamba dakika ya 45.

Kipindi cha pili Pamba iliingia kama nyuki na kufanya mashambulizi mfululizo na kufanikiwa kupata mabao mawili ya haraka yaliwekwa wavuni na Julius dakika ya 46 na Kevin John dakika ya 47.

Hata hivyo Mashujaa ilijaribu kupambana kutaka kusawazisha mabao hayo, lakini mambo yaliwawia magumu na kujikuta dakika 90 zikimalizika kwa wenyeji Pamba kuondoka kifua mbele.

Kwa matokeo hayo, Mashujaa FC wanabaki na pointi zao tatu, huku Pamba wakifikisha alama sita baada ya kushuka uwanjani mara tatu kwa timu zote.

Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo Green Warriors ikiwa nyumbani imekubalia kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Dodoma FC.