Pamba balaa, yafukuza mwizi kimya kimya

Tuesday November 14 2017

 

By CHARLES ABEL

LICHA ya timu za Alliance, Biashara na Dodoma FC kupewa nafasi kubwa ya kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao kutokea Kundi C la Ligi Daraja la Kwanza, huenda mambo yakabadilika dakika za mwishoni kutokana na Pamba kukimbiza mwizi kimya kimya.

Pamba iliyoanza mbio hizo msimu huu kwa kusuasua, imegeuka tishio kutokana na kupata ushindi kwenye mechi tatu mfululizo hivi karibuni na kuzisogelea Alliance, Dodoma na Biashara zilizo Tatu Bora na huenda ikazitawanya.

Baada ya kupata pointi tatu tu katika michezo sita ya mwanzoni iliyocheza dhidi ya timu za Dodoma FC, JKT Oljoro, Biashara United, Transit Camp, Toto Africans na Alliance Schools, timu hiyo ya Mwanza ilifufuka na kupata ushindi katika mechi zilizofuata dhidi ya Rhino Rangers, Dodoma FC na JKT Oljoro jambo lililoifanya isogee hadi nafasi ya nne ikiwa na pointi 12 ambazo ni saba pungufu ya vinara Alliance.

“Siri ya mafanikio ni mazoezi tu. Tunafanya ya kutosha na wachezaji tumewasaidia waweze kujiamini wanapokuwa na mchezo. Unajua unapopoteza au kutoka sare hali ya kujiamini inapotea, ni tofauti na unaposhinda,” alisema Kocha wa Pamba, Venance Kazungu.

“Nawaomba wakazi wa Mwanza waendelee kutupa sapoti na kutushauri pia. Binafsi niko tayari kushauriwa na mtu mwingine yeyote anayejua mpira soka kwani, milango ya mawazo iko wazi. Nia ni kuifanya Pamba itinge Ligi Kuu.”