Pamba FC watatu ndani, tisa nje

Thursday December 7 2017

 

By Masoud Masasi

Mwanza. Pamba FC “TP Lindanda” si watu wa mchezo mchezo wameamua kusafisha kikosi chao kwa kuwatema wachezaji tisa katika dirisha hili dogo la usajili na kupanga kusajili watatu pekee.

Pamba ipo Kundi C katika Ligi Daraja la Kwanza ikiwa nafasi ya nne na pointi 12, kuna uwezekano ikashindwa kupanda daraja msimu huu.

Wachezaji waliotemwa katika kikosi hicho mabeki Rashid Kondo, Steven Maganga, washambuliaji Julias Msumari Miraji Salehe, John Masiroli.Wengine ni viungo Nelson Kagawa, Juma Dede na Nassoro Kibesa.

Afisa Habari wa klabu hiyo, Johnson James alisema wachezaji hao wameachwa kwa sababu mbalimbali ikiwepo nidhamu na kiwango chao kushuka.

James alisema wamepunguza wachezaji hao kwani walisajili 29 hivyo wamewatema tisa ambapo watasajili watatu na kufanya wawe na nyota 23 ambao watapambana kuirejesha Ligi Kuu timu hiyo.

“Kwanza hawa wachezaji tisa tuliowatema wengi wao walishaondoka ndani ya timu na wengine kiwango chao kilishuka hivyo tukaona tuwe na kikosi kikosi chenye nyota wachache, lakini wawe wapambanaji,”alisema James.

Afisa huyo alisema kwa sasa timu hiyo ipo katika mazoezi makali kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi hiyo itakayoanza kurindima Desemba 16.