Pamba FC wana jambo lao huku

Muktasari:

Pamba inatupa karata yake ya kwanza kesho Jumamosi dhidi ya AFC katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza utakaopigwa dimba la Nyamagana jijini Mwanza.

PAMBA FC imesisitiza kuwa ili kuhakikisha wanafikia lengo lao la kupanda Ligi Kuu msimu ujao, wanahitaji ushindi kesho Jumamosi dhidi ya Arusha FC na kuanza rasmi safari yao ya matumaini.

Pamba ambayo imedumu Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa miaka 20 tangu waliposhuka daraja mwaka 1990, wanatarajia kushuka dimbani kuwakaribisha AFC ya jijini Arusha, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Nyamagana jijini hapa ikiwa ni mechi ya kwanza ya ligi hiyo.

Akizungumza jijini hapa, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ulimboka Mwakingwe amesema hawatafanya makosa ambayo yataigharimu timu kutofikia malengo ya kupanda Ligi Kuu.

Amesema katika kuhakikisha wanafanya kweli, wamejiandaa kushinda mchezo wao wa kwanza dhidi ya AFC ikiwa ni mwanzo wa harakati zao za kusaka tiketi ya kucheza Ligi  Kuu msimu ujao.

 "AFC naijua kwa sababu nimeifundisha, kwa sasa naitumikia Pamba FC ninachohitaji ni kuona tunaanza kwa ushindi, nimewaandaa vyema wachezaji na matumaini yangu ni kubaki na alama tatu" amesema Mwakingwe.

Nahodha wa timu hiyo, Majaliwa Shaban amesema mara kadhaa wachezaji wamekuwa na vikao kujadili namna ya kuisadia timu kupanda daraja, hivyo kwa sasa ni muda wao kusema inatosha kucheza FDL.

"Kisaikolojia, kiushindani tuko fiti, huu ni muda wa kupambana kuona tunafikia maazimio yetu ya kupandisha timu Ligi Kuu, tunasema miaka 20 ya FDL inatosha" amesema nyota huyo wa zamani wa Mbeya City.

Mchezaji wa zamani wa timu za RTC Mwanza, Toto Africans na Pamba FC, Munga Lupindo amesema msimu huu ni zamu ya Pamba kucheza Ligi Kuu kwani wamejiandaa kutoa sapoti ya aina yoyote ili kurejesha heshima ya Klabu hiyo.

"Sisi wachezaji wa zamani tuko pamoja na timu yetu, tumejiandaa kuungana nao kuona msimu ujao inarejea Ligi Kuu, niwaombe wadau na mashabiki kesho waje kwa wingi," amesema Lupindo ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Wilaya ya Nyamagana (NDFA).