Pamba FC inasaka pointi saba tu

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Kisaka alisema kutokana na ushindani na ratiba jinsi ilivyo, watapambana kusaka pointi saba katika mechi tatu watakazocheza ugenini.

MWANZA.KOCHA wa Pamba FC, Ally Kisaka amesema katika mechi tatu wanazotarajia kucheza ugenini, anahitaji pointi saba tu ambazo zitaiweka mazingira mazuri klabu yake katika mbio za kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Timu hiyo ambayo imetoka kupata ushindi mfululizo kwenye mechi mbili ilizocheza kwenye Dimba la Nyamagana Mwanza dhidi ya Dodoma na juzi Jumamosi iliilaza Transit Camp bao 1-0 lililofungwa na Geofrey Julias na sasa wanatarajia kucheza michezo mitatu ugenini.

Kikosi hicho kilichowahi kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano mwaka 1990, kitaanzia mkoani Tabora kukipiga na Mgambo Shooting, kisha kuifuata Mashujaa ya Kigoma na baadaye kuwavaa Polisi Tanzania huko Kilimanjaro.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kisaka alisema kutokana na ushindani na ratiba jinsi ilivyo, watapambana kusaka pointi saba katika mechi tatu watakazocheza ugenini.

Alisema iwapo watafanikiwa kupata alama hizo zitawasogeza katika nafasi nzuri kwani mechi za nyumbani haziwapi presha sana.

Aliongeza kutokana na mwenendo walionao kuna kila dalili za timu hiyo kupanda Ligi Kuu msimu ujao kwani kikosi chake kinajituma.