Pale Gor Mahia ‘Kogalo’ ni twa twa twa

Thursday November 28 2019

Gor Mahia-ligi kuu-WACHEZAJI-MWENYEKITI-MICHEZO BLOG-MWANASPORT-MWANASPOTISOKA-

 

By Thomas Matiko

Nairobi, Kenya.IKO shida! Iko shida buda pale Gor Mahia. Mangira pale kwa sasa hivi ni twa twa twa. Pamoja na kwamba wamegandia kileleni mwa jedwali la ligi kuu wakiwa na mechi mbili za viporo, taarifa zilizopo ni sasa klabu hiyo ipo kwenye tishio la kukimbiwa na wachezaji wake.

Tatizo ni mabingwa hao watetezi wa ligi kuu wamesota hadi wanatia aibu licha ya kulipwa mamilioni ya pesa  kutoka kwa ushiriki wao wa mashindano ya CAF msimu uliopita.

Wanacholia ni kumkosa mdhamini tangu Sportpesa alipoamua kuinua zake. Sasa wachezaji wa Gor hawajalipwa kwa mwezi wa tano sasa ukiwa unaingia.

Tayari Mwenyekiti wa Gor, Ambrose Rachier kathibitisha kuna baadhi ya wachezaji wameshampa notisi wataondoka.

Mmoja wao ni  beki Maurice Onjwang waliyemsajili kutoka Western Stima ambaye Rachier kathibitisha kupokea notisi yake ikimwarifu anapania kuondoka itakapofikia Desemba 6.

Mlinzi huyo anasema kama hatakuwa amelipwa mshahara wake wote kufikia tarehe hiyo basi atalazimika kuvunja mkataba wake na Gor kwa mujibu wa kanuni na sheria za FIFA. Sheri za FIFA zinamruhusu mchezaji kuvunja mkataba wake baada ya miezi mitano kama hajapokea mshahara wake.