Pacha za mabao Ligi Kuu England

Muktasari:

Hapa yamechukuliwa mabao yaliyofungwa na wachezaji hao pacha baada ya kucheza pamoja ndani ya uwanja unaozidi dakika 5,000. Hizi pacha noma, ile ukikutana nazo tu uwanjani basi wavu wako lazima uguswe.

LONDON, ENGLAND . WANASEMA soka ni mchezo unaochezwa kitimu.

Sawa, mastraika wamekuwa wakipewa sifa sana kutokana na kazi yao ya kutumbukiza mipira nyavuni, lakini kazi yao hiyo isingewezekana kama wasingekuwa na msaada wa wachezaji wengine 10 waliopo nyuma yao.

Wakati mwingine mambo yanakuwa matamu zaidi kwa mashabiki kushuhudia wachezaji wawili wanaoelewana vyema kwenye timu na kuchangia kufunga mabao mengi, huku ushirikiano wao ukiwaacha kwenye wakati mgumu mabeki wa timu pinzani.

Mastaa hao wawili wanapokuwa kwenye ubora sawa, kwa maana ya kufunga mabao na kutengenezeana kwa pasi za mwisho, jambo hilo linakuwa limewapendeza makocha kwa sababu wanakuwa na furaha kwa kuwa wamefanikiwa kutengeneza kombenisheni matata.

Mfano mzuri kwenye kikosi cha Arsenal kuna pacha moto kabisa kwa kufunga mabao ile ya Alexandre Lacazette na Pierre-Emerick Aubameyang au kama ile iliyokuwa klabuni Liverpool wakati wa Kocha Brendan Rodgers iliyowahusisha Luis Suarez na Daniel Sturridge.

Lakini, umeshawahi kujiuliza ni pacha gani hatari zaidi kwa kufunga mabao iliyowahi kutokea kwenye Ligi Kuu England na kutesa mabeki wa timu pinzani? Wala usipate shida, mambo yote haya hapa.

Hapa yamechukuliwa mabao yaliyofungwa na wachezaji hao pacha baada ya kucheza pamoja ndani ya uwanja unaozidi dakika 5,000. Hizi pacha noma, ile ukikutana nazo tu uwanjani basi wavu wako lazima uguswe.

5) Torres na Gerrard – Liverpool, mabao 81

Mastaa wawili waliokuwa moto walipokuwa pamoja huko Anfield, kiungo Steven Gerrard na straika Fernando Torres walitengeneza kombinesheni matata sana ndani ya uwanja iliyokuwa na kazi moja tu kuipigia mabao Liverpool. Wawili hao kwenye mechi walizocheza pamoja wamehusika kwenye mabao 81 na kufanya kuwa moja ya pacha kali kabisa zilizowahi kutokea kwenye historia ya Ligi Kuu England. Ubora wao wote wawili hao walishindwa kuipa Liverpool ubingwa wa ligi hadi hapo Torres alipohamia Chelsea kwa Pauni 50 milioni na kuvunja kombinesheni hiyo.

4) Mo Salah na Sadio Mane – Liverpool, mabao 89

Jurgen Klopp anatamba tu kwenye kikosi chake cha Liverpool. Msimu uliopita alishindwa kidogo tu kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England kabla ya kwenda kunyakua ubingwa wa Ulaya na msimu huu kinachoonekana ni wakati tu ndio uliobaki kujibebea ubingwa wa ligi. Chama lake limeweka pengo la pointi 22 kileleni, huku akiwa na huduma nzuri kabisa kutoka kwa mastaa wake, Mohamed Salah na Sadio Mane, waliotengeneza kombisheni safi ambapo kwa dakika walizokuwa pamoja ndani ya uwanja wamehusika kwenye mabao 89 na kuwa moja ya pacha hatari kwenye kufunga mabao.

3) Aguero na Sterling – Man City, mabao 100

Pep Guardiola amekuwa na wakati mzuri kwenye kikosi cha Manchester City kabla ya mambo kutibuka msimu huu na kuonekana kuwa magumu kwa upande wake. Kwenye kikosi chake ambacho alibeba ubingwa wa Ligi Kuu England kwa misimu miwili mfululizo, kuna huduma ya fowadi wawili wanaoelewa vyema na kufunga mabao kwa kadri wanavyotaka. Fowadi hao ni Sergio Aguero wa Argentina na Raheem Sterling wa England, ambapo wamehusika kwenye mabao 100 na hivyo kuwa moja ya pacha hatari kwa kutupia katika ligi hiyo. Pacha hao wawili wanapambana kuhakikisha Man City inamaliza ndani ya Top Four msimu huu licha ya kufungiwa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu miwili.

1) Henry na Pires – Arsenal, mabao 162

Ni wakati huo Arsenal ilipokuwa moto uwanjani na nguvu ya kupambania mataji chini ya kocha wao Arsene Wenger kwenye kikosi chao kulikuwa na kombinesheni hatari ya mastaa wawili wote Wafaransa, Thierry Henry na Robert Pires. Katika dakika zao za pamoja walizokuwa uwanjani kuitumikia Arsenal, wakali hao walihusika kwenye mabao 162 na kufanya kuwa moja ya pacha hatari kuwahi kutokea kwenye Ligi Kuu England ambayo ilitesa kwa kufunga mabao lukuki. Henry na Pires walicheza kwa mafanikio makubwa kwenye kikosi hicho cha The Gunners na kuacha kumbukumbu tamu kabla ya kutimka.

2) Kane na Son– Tottenham, mabao 102

Bahati mbaya kwa Jose Mourinho huko kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur ni kwamba ameshindwa kupata muda wa kuwashuhudia mastaa wake wawili hatari kwenye safu ya ushambuliaji, Harry Kane na Son Heung-min wakicheza pamoja. Washambuliaji wote hao wawili kwa sasa wanakosekana katika kikosi cha Spurs kutokana na kuwa majeruhi, lakini katika dakika ambazo walikuwa pamoja ndani ya uwanja kuitumikia timu hiyo wamehusika kwenye mabao 102.