Pacha wa Haruna Moshi 'Boban' ampa dili Ajib

Muktasari:

  • Costa ambaye anacheza nafasi ya ushambuliaji katika kikosi hicho akiwa ni pacha wa Haruna Moshi 'Boban' anaamini Tanzania ni nchi yenye vipaji vingi vya soka.

Dar es Salaam. Mzungu wa African Lyon, Mfaransa Victor Da Costa amesema nafasi pekee  kwa wachezaji wa Kitanzania kucheza soka ya kulipwa barani Ulaya ni kufanya vizuri kwenye timu ya Taifa 'Taifa Stars'.
Costa ambaye anacheza nafasi ya ushambuliaji katika kikosi hicho akiwa ni pacha wa Haruna Moshi 'Boban' anaamini Tanzania ni nchi yenye vipaji vingi vya soka.
"Inawezekana mawakala wengi wa soka wanaibeza Tanzania kwa sababu ipo chini kwenye viwango vya ubora wa soka duniani. Kama wangekuwa kuanzia nafasi ya 80 kupanda juu, ingesaidia.
"Vinginevyo itaendelea kutumika nguvu kubwa, muda mfupi ambao nimekuwa hapa nimegundua hii nchi inawachezaji wengi wenye uwezo wa kucheza hata kwenge ligi ya nyumbani Ufaransa 'France Ligue 1'," alisema Costa.
Timu ya Taifa 'Taifa Stars' ina wachezaji wengi wanaocheza soka la Tanzania lakini mashabiki wanaamini uwezo wao ni wa juu kama, Ibrahim Ajib wa Yanga na Shiza Kichuya.
Costa ambaye kimwonekano anafanana na mshambuliaji wa Chelsea, Olivier Giroud ni mzaliwa wa  Ureno, aliyekua na kuchukua uraia wa  Ufaransa.
Mshambuliaji huyo amezichezea klabu kadhaa kabla ya kutua Tanzania ambazo ni Southern United, Dunedin Technical AFC, Otago United za New Zealand na Magni ya Iceland.