PSG yapiga chini ofa ya Barca kwa Neymar

Muktasari:

Neymar amekuwa akihusishwa na kurudi Barcelona, pia akitakiwa kwa nguvu na Real Madrid ambayo kwa sasa imeonekana kulegeza kamba kutokana na ujio wa Eden Hazard kutoka Chelsea.

MIAMBA ya Jiji la Paris na Ligi Kuu ya Ligue 1, PSG wamepiga chini ofa iliyowekwa mezani na Barcelona kwa ajili ya kumchukua nyota wa timu hiyo, Mbrazil, Neymar Jr.

Pamoja na PSG kuwa tayari kumruhusu mshambuliaji wao huyo kuondoka klabuni hapo, lakini wanachotaka wao ni dau la maana litakalofikia lile la Pauni 203 milioni walilotoa kumpata nyota huyo akitokea Barcelona.

Hata kama Barca watamalizia dau lote hadi kufikia mwaka ujao kama inavyodaiwa ili kumchukua jumla, lakini PSG hawaamini kama mabingwa hao wa La Liga watakamilisha malipo hayo kitu ambacho kimewafanya wasite kumwachia nyota huyo.

Neymar amekuwa akihusishwa na kurudi Barcelona, pia akitakiwa kwa nguvu na Real Madrid ambayo kwa sasa imeonekana kulegeza kamba kutokana na ujio wa Eden Hazard kutoka Chelsea.

Neymar amekuwa na hamu ya kurudi kwenye Barcelona ambako alicheza kwa kiwango kikubwa sambamba na Lionel Messi na Luis Suarez.